DC Msulwa awataka vijana kujiunga na vikundi wapate mikopo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Bakari Msulwa, akizungumza na Wananchi katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Mji Mkuu, Sabasaba pamoja na Kata ya Kingo Manispaa ya Morogoro.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro,
Mhe. Bakari Msulwa, amewataka Vijana
waliopo katika makundi yasiyo rasmi kujiunga katika vikundi ili waweze kupatiwa
mikopo itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Hayo ameyasema leo Septemba
07, 2020 kwenye Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa
Kata ya Mji Mkuu, Sabasaba pamoja na Kata ya Kingo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa
habari kwa nyakati tofauti tofauti wakati wa ziara hiyo, amesema Vikundi vingi vya Vijana visivyo katika
mfumo rasmi vimekuwa havikopesheki kwa sababu hawajajiunga katika vikundi
vinavyotambulika na Manispaa zao na kutokuwa na Katiba.
“Ili kuendana na sera ya
Serikali ya viwanda, vikundi hivi ambavyo havipo rasmi huu ni wakati sasa wa wao
kukaa pamoja kutengeneza katiba na kupata usajili, hivyo baada ya usajili sasa
vitakuwa rasmi vinatambulika na watakuwa
hawana budi kujiunga katika
vikundi vidogo ili kupata mikopo itakayowasaidia kuanzisha viwanda vidogo jambo
ambalo litawasaidia kuongeza kipato na ajira kwa watu wengine ,” Amesema DC
Msulwa .
DC Msulwa, amesema ili
mjasiriliamali aweze kufanikiwa lazima awe na nidhamu na fedha anayopata na si
kuitumia hovyo kwani itasababisha kuyumba kwa biashara na hatimaye kufilisika.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse , amesema ili Vijana
wafanikiwe lazima waondokane na tabia ya kuwa na vikundi ambavyo sio rasmi na
kuwa katika vikundi rasmi vinavyotambulika ili viweze kujikwamua kiuchumi na kujijengea ajira kuliko
kusubiri kuajiriwa.
Post a Comment