Header Ads

TARURA watakiwa kuweka wazi utaratibu wa vibali vya kushushia mizigo Barabarani.

 

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, akisalimiana na Mzee maarufu Manispaa ya Morogoro leo mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi Kata ya Sabasaba.


Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John , akizungumza kwa ajili ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua  kero za Wananchi Kata ya Kingo.

Mhandisi wa TARURA Manispaa ya Morogoro, James Mnene, akijibu na kufafanua kero ya Wafanyabiashara wa Mahindi ya Kuchoma  waliopo eneo la Fire Kata ya Sabasaba   kuhusu  upatikanaji wa vibali vya kushusha mizigo barabarani.


Wananchi wakifuatilia kwa makini Mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro wa kusikiliza na kutatua kero Kata ya Kingo.


MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amewataka TARURA Manispaa ya Morogoro kuhakikisha inaweka wazi juu ya suala la upatikanaji wa vibali vya kushusah mizigo katika barabara za ndani.

Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 07, 2020 kufuatia hoja ya mmoja wa wafanyabiashara aliyedai kwamba wanazuiwa kushusha mizigo yao kwa kukosa kibali cha ushushaji.

Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Msulwa, amemtaka Mhandisi wa TARURA Manispaa ya Morogoro, James Mnene, kuweka viwango vya tozo ya upatikanaji wa viabali hivyo ili iwe rahisi ya wafanyabiashara wanaotaka kushusha mizigo yao wafahamu na kuepusha usumbufu.

“”Hili nafikiri leo tunalipatia ufumbuzi, najua ipo sheria ya upatikanaji   wa vibali vya ushushaji wa mizigo lakini kama hili jambo lenu kwa nyie wafanyabishara wa mahindi ya kuchoma linaleta shida, namuagiza hapa Mhandisi ahakikishe anawapa maelekezo na utaratibu wa sheria zinazoruhusu ubebaji wa tani za mizigo katika barabara zetu za mitaani  pamoja na bei ya vibali hivyo ili wale wanaoingia mjini wanaposhusha  mzigo wajue mzigo huu unashuwaje na unalipiwa vipi kuliko usumbufu huu mnaoupata”” Amesema DC Msulwa.

Licha ya kutoa maagizo hayo, lakini amemuagiza Mhandisi huyo kuhakikisha kwamba katika utaoaji wa viabali hivyo vya ushushaji wa mizigo waanze kubainisha barabara zenye masoko.

“Lengo la kubainisha suala hili la ushushaji wa mizigo kwa kutoa vibali litasaidia sana kupunguza misongamano isiyo ya kilazima kwa wateja kwani kitendo cha kutaka wafike Ofisini kwa TARURA ni msongamano hivyo kila mmoja afahamu taratibu na sheria ili maisha yaendelee na biashara ziendelee kufanyika kwa ajili ya kujenga uchumi wetu”” Ameongeza DC Msulwa.

Akijibu juu ya hoja hiyo, Mhandisi wa TARURA Manispaa ya Morogoro, James Mnene, amesema agizo la Mkuu wa Wilaya amelipokea na watalifanyia kazi haraka iwezekanavyo bila ya uonevu wa aina yoyote kwa wateja wao.

“Agizo tumelipokea shida iliyokuwepo ilikuwa suala zima la uelewa na mawasiliano kwa wafanyabiashara wetu lakini tutahakikisha tunalifanyia kazi kwa mujibu wa sheria zetu za TARURA ili huduma ziendelee” Amesema Eng. James Mnene.

Mbali na suala la vibali, DC Msulwa, ameenda mbali zaidi na kuwataka Kampuni iliyopewa dhamana ya usafishaji wa mji na Manispaa ya Morogoro, Kampuni ya Kajenjere kuweka ratiba maalumu ya uzoaji wa taka majumbani jambo ambalo  limekuwa likilalamikikiwa na Wananchi kwani wengi wao taka zinabakia nyumbani kwa kutokujua muda maalumu wa takataka hizo kuchukuliwa.

“Hili pia nataka niliweke wazi, Mji wetu unakuwa kwa kasi sana, nawapongeza sana Manispaa ya Morogoro kwa kuleta Kampuni hii sasa angalau taswira ya Mji inaonekana , tunakwenda kuwa Jiji lazima usafi ufanyike kweli, lakini pia nyinyi Kajenjere wekeni ratiba za Mitaa yenu ya kazi, kuna wengine wanakwenda kazini, mkiweka ratiba hata yule anayeenda kazini utamsaidia kujua lini taka zinaondoka kwake, mkifanya hivyo hata hizi kero ndogondogo zitapungua “ Amesema DC Msulwa.

Aidha, suala la Ofisi ya Kata ya Kingo hakuliacha kwani amemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuhakikisha kwamba Kata zote zinakuwa na Ofisi za kudumu na kutaka kupata orodha ya Kata ambazo hazina Ofisi, zenye Ofisi na zile na mipango ya Manispaa kujenga Ofisi ikoje.

Hata hivyo  hakulifumbia macho suala la bili za maji kuongezeka, hivyo ameugiza Uongozi wa MORUWASA chini ya Mkurugenzi wake kufanya vikao na Wananchi na kupitia  mita hizo vizuri ili kubaini tatizo badala ya kuacha Wananchi kuendelea kuteseka na kulalamika.

Mwisho , amewataka Wananchi kufanya Kampeni za kistaarabu katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Ubunge na Madiwani Oktoba 28, 2020 na kuwaomba Wananchi kusikiliza sera vizuri za wagombea na hatimaye kufanya maamuzi yenye busara yatakayoweza kuwapatia maendeleo kwa kipindi  cha miaka 5 ijayo.


 

 

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.