DC MSULWA AWATAKA WATUMISHI KUFANYA KAZI KWA UADILIFU .
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa , amewataka watumishi wa umma Wilaya ya Morogoro kufanya kazi kwa weledi na uadilifu na kuwaasa wasikimbie maeneo yao kazi badala yake wawe chachu ya mabadiliko na utatuzi wa changamoto wanazokutana nazo katika maeneo yao.
Hayo ameyazungumza leo Juni 25,2020 wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mstaafu wa Morogoro, Mhe. Regina Chonjo kwenye ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro.
Msulwa, amesema watumishi wa umma wana maarifa hivyo wanapaswa kutumia maarifa hayo kukabiliana na changamoto zinazowakabili badala ya kuhama maeneo ya kazi kwa kuwa Wananchi wanawahitaji kwa ajili ya kuwapa huduma wanazostahili.
Amesema vyema kila Halmashauri kujiwekea utaratibu wa kuwapongeza watumishi wanaotimiza wajibu wao vizuri ili kuongeza morali ya utendaji kazi kwa watumishi na kwa wale wanaokiuka maadili ya utumishi na kuwa wazembe katika kazi kupewa onyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa Umma.
“Utumishi wa umma ni fursa, utumishi wa umma ni fursa fanyeni kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu maana dunia inabadiilika na ndiyo maana tunasisitiza waajiri watoe mafunzo ya mara kwa mara ili watumishi waendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia,niwaombe muepuke uwizi na mfanye kazi kwa uadilifu wa hali ya juu na kuacha kufanya kazi kwa maigizo lakini haya yote yatakuja endapo tutafanya kazi kwa ushirikiano ” Amesema Mhe. Msulwa.
Aidha, amewakumbusha watumshi wa umma muelekeo wa serikali ya awamu ya tano katika kujenga misingi ya utumishi wa umma.
Amesema kuwa serikali inatarajia kuwa na watumishi wenye uadilifu uliotukuta katika jamii na utoaji huduma kwa wananchi, watumishi wanaowajibika kwa serikali nawananchi, nidhamu ya kazi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, ndio dira ya serikali na itasimamia kuona kuwa utekelezaji unafanyika.
""Kila mmoja atimize wajibu wake, migogoro kwa kiasi kikubwa inazuirika kwani Serikali yetu ina mfumo mzuri kuanzia ngazi za chini hadi za juu, baadhi ya wataalamu wanakuwa vyanzo vya migogoro huku wananchi wakihangaika bila sababu , lakini pia wananchi hawapewi taarifa kwa wakati hili sio jambo jema, kiongozi mzuri ni yule aliye katika suluhu ya matatizo na sio sehemu ya matatizo, niwaombe wataalamu msisubiri viongozi wa kisiasa waje watatua kero hizo fanyeni kazi na muwe makini katika kutatua migogoro kwa kutumia taaluma zenu ili wananchi muwape huduma bora na wafurahie matunda ya kuwa na Uongozi katika sehemu husika " Ameongeza Mhe. Msulwa.
Hata hivyo, amesema kuwa ni jukumu la kila mkuu wa Idara na kitengo kusimamia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma ili kuweza kuleta maendeleo chanya kwa watu anawasimamia na kuondoa kero na malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara kwani kuna matatizo mengine ni madogo ambayo yako ndani ya uwezo wa mkuu wa idara au kitengo kuweza kuyatatua.
Alimalizia kwa kuwapongeza watumishi wa Halmashauri ya Morogoro kwa uwajibakaji na utendaji wao kazi uliotukuka na kuwataka kuendelea na moyo huo huo wa kuwatumikia wananchi wa Manispaa ya Morogoro ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi kuloingana na sekta zao.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa nasaha yake pamoja na maagizo kwa Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao katika maeneo yao ya kazi.
Post a Comment