Header Ads

DAS WILAYA YA MOROGORO ATOA WITO KWA TAASISI MBALIMBALI KUJITOLEA KUSAIDIA WATU WENYE UHITAJI MAALUMU.

Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John, akiwa amembeba mtoto aliyetelekezwa na Wazazi wake mara baada ya kumfikisha katika Makao ya kulelea Watoto yatima na wenye mazingira magumu ya Mgolole katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Juni 16, 2020.
Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Sidina Mathias (kulia) akimsindikiza Katibu Tawala (kushoto) wakati wa kutoka katika Makao ya Mgolole.
Katibu Tawla Wilaya ya Morogoro, Ruth John (katikati) akiwa pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe wakimkabidhi zawadi ya vyakula Mkurugenzi wa Makao ya kulelea yatima Mission To The Homeless  yaliyopo Kata ya Mkundi , Robert Simba wakati walipotemebelea katika makao hayo katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
Baadhi ya Watoto wakiwa makini kumsikiliza Katibu Tawala akiwapatia elimu .

Vyakula vikionekana mbele 



Viongozi wakikagua bidhaa zinazozalishwa na Makao ya Kulelea watoto yatima ya Mission To The Homeless.


KATIBU Tawala Wilaya ya Morogoro, Ruth John, ametoa wito kwa taasisi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara na watu wenye mapenzi mema kujitolea kusaidia watu wenye uhitaji maalumu kwani kwa kufanya hivyo ni kutimiza amri kuu ya upendo ya Mwenyezi Mungu isemayo pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi.

Ruth ameyasema hayo  akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo wakati akitoa misaada mbalimbali kwa Makao ya  kulelea watoto wenye mahitaji maalumu Mgolole pamoja na Mission To The Homeless  katika hafla fupi ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika Juni 16,2020.

DAS Ruth , amekabidhi  misaada hiyo kwa wawakilishi wachache wa watoto hao walioongozana na baadhi ya walezi wao, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuepuka mikusanyiko ya watu isiyo lazima kutokana na janga la ugonjwa wa mafua makali ya CORONA.


 "Mkuu wa Wilaya yenu anawapenda sana , ameniagiza nije kuwaona na kuwaletea kile alaichokiandaa , kwahiyo niseme kuwa Serikali yenu  chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli inawapenda sana , kikubwa mjisikie huru kama walivyo watoto wengine, msirudi nyuma kwani kuondokewa na Wazazi au kukosa malezi ya wazazi isiwe kigezo cha kuwarudisheni nyuma mnatakiwa msongo mbele ili nanyi myafikie malengo mliyojiwekea" Amesema Ruth.

Aidha amesema kuwa wapo watu ambao wamekuwa wakitoa misaada kwa watoto au watu ambao wamekua wakizunguka mitaani na kuomba misaada kuwa, huo sio utaratibu mzuri na kusisitiza kuwa ni vyema mtu unapokuwa na tatizo na unahitaji msaada kufika katika ofisi za serikali na kuonana na Maafisa Ustawi ili waweze kushauri njia bora za kuweza kusaidiwa.

Kwa upande wa Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe, amesema ni vyema jamii ikawiwa kuchangia makundi ya watoto wenye mahitaji maalumu vikiwemo vituo vya watoto yatima kwani kundi hili linahitaji msaada wa kuwa karibu zaidi na jamii kutokana na wengi wao kupotelewa na wazazi au kutelekezwa na ndugu zao.

Mwanakatwe, amesema kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya ndugu wa watoto waliopo kwenye vituo na jamii kwa ujumla kutokuona umuhimu wa kuwatembelea na kuwajulia hali watoto licha ya elimu ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa kuona kuwa jukumu hilo ni la jamii kwa ujumla na sio serikali peke yake au taasisi binafsi.

“Pindi inapotokea mtoto amefiwa na wazazi ndugu wamekuwa wakiwaleta watoto vituoni, watoto wakishapokelewa ndio mwisho wa ndugu wa mtoto husika kufika kituoni kumjulia hali au pengine hata kusaidia mahitaji mbalimbali, jambo hili linasikitisha sana mtoto anakua pasipo hata kufahamu ndugu zake wakati hii ni haki ya mtoto kisheria.”Amesema Mwanakatwe.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Morogoro, Sidina Mathias, ametoa  rai kwa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto kuhakikisha kuwa pindi wapatapo taarifa au wanapoletewa watoto waliotelekezwa au kupotelewa na wazazi ni vyema kufikisha taarifa kwa maafisa ustawi kabla ya kuwapokea na kuanza kuwahudumia katika vituo vyao lengo ikiwa ni kuhakikisha kuwa Maafisa ustawi wanashirikishwa ili waweze kufuatilia kwa undani taarifa za watoto husika lakini pia kujua taarifa za awali za mtoto husika kwani kumekuwa na tabia ya wazazi kutelekeza watoto wakiamini kuwa watasaidiwa vyema kwenye vituo vya kulelea watoto jambo ambalo sio sahihi.


Sidina amesema kuwa kwa mujibu wa sheria namba 21 ya mwaka 2009 kifungu namba 94 kinaeleza wajibu wa Halmashauri kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

 Misaada aliyotoa Katibu Tawala ni pamoja na mchele kilo 200, mafuta ya kula lita  80 na Sukari Kilo 50 kwa makao yote mawili.





No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.