DC CHONJO AWAHAMASISHA WAJASIRIAMALI WADOGOWADOGO KUCHUKUA VITAMBULISHO.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Regina Chonjo,akihamasisha uuzwaji wa Vitambulisho vya Wajasiriamali katika mnada wa Soko la Sabasaba Manispaa ya Morogoro. |
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ametoa wito kwa wajasiriamali wadogo wadogo wasiozidi kipato cha milioni nne kwa mwaka kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vya wajasiriamali wadogo wadogo vitambulisho ambavyo vimetolewa na Mheshimiwa Rais lengo ikiwa ni kuwajali wajasiriamaqli hao.
Wito huo ameutoa leo Juni 07,2020 wakati wa kampeni ya kuhamasisha wajasiriamali hao kuchukua vitambulisho hivyo katika Mnada wa Sabasaba Manispaa ya Morogoro ambapo licha ya kutoa hamasa lakini pia aligawa vitambulisho kwa wajasiriamali zaidi ya 100 kwa wajasiriamali wadogowadogo wa Mnada wa Sabasaba kwa shilingi 20,000/=.
Akizungumza kuhusu vitambulisho hivyo, DC Chonjo, amesema kuwa vinampa fusra mjasiriamali kufanya biashara ya aina yoyote isiyozidi millioni nne kwa mwaka eneo lolote hapa nchini lakini pia kinamsaidia kufanya biashara eneo lolote kwa uhuru huku akiaminika katika maeneo atakayofanyia biashara kupitia uwepo wa kitambulisho hicho.
Aidha, amewataka watendaji wa kata, watendaji wa vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji kuongeza kasi ya uhamasishaji na kuwatambua wajasiriamali wanaostahili vitambulisho ili waweze kupatiwa huku akiwasisitiza wafanyabiashara mbalimbali kuwa yapo makundi mawili ambayo ni mfanyabiashara kuwa na namba ya mlipa kodi TIN au kuwa na kitambulisho cha mjasiriamali na kwamba kila mfanyabiashara lazima awe na utambulisho kati ya TIN au kitambulisho na kwa atakayebainika kutokuwa na utambulisho wowote hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
"Nimelazimka kuwafuata wajasiriamali wadogo katika maeneo yao ya biashara ili kuwapatia elimu ya kutosha kuhusu faida ya kuwa na kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo, hii imetokana baada ya kubaini wengi wao hawajahamasishwa vya kutosha ya kutambua manufaa watakayopata, haya maendeleo mnayoyaona yanatokana na Kodi zetu , Sasa mkikwepa Kodi hizi ambazo zina gharama ya chini sio haki, hamumtendei Rais wetu haki maana aliwatambua na nyie mnatakiwa mjitambue, pesa hizi zinaboresha miundombinu, barabara, Hospitali, Shule , huduma za maji , umeme n.k yote haya bila sisi kuchangia hatutaweza kufikia lengo la Rais wetu katika kuelekea Uchumi wa Kati na Tanzania ya Viwanda"Amesema DC Chonjo.
Akibainisha aina za biashara na wajasiliamali wanaostahili kupata vitambulisho, Afisa Tarafa wa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako, amesema wajasiriamli wanaostahili kuwa na vitambulisho ni mama/baba lishe, boda boda, wasusi wa nywele, vinyozi, mafundi viatu, wauza CD na kanda za video, wanaoingiza nyimbo kwenye memory card, wakaanga chips, wauza mbogamboga, waosha magari, wapaka rangi kucha, wauza dawa za mbu na za asili, wakodishaji baiskeli, wauza maji,soda, mafundi seremala, wasukuma maguta/mikokoteni, wauza matunda,mafundi saa au simu, watembeza biashara mikononi na wengine wenye biashara kama hizo.
Hata hivyo, amesema ,ili kufanikicha zoezi hilo Madiwani ni watu muhimu kwa vile ni wawakilishi wa wananchi wao katika Kata wanazotoka , hivyo ni vyema wakajitokeza kuhamasisha vijana , akina mama na watu wengine walengwa wa mpango huo ili wanufaika kutobughudhiwa wanapokuwa kwenye biashara zao.
“ Nawaomba Madiwani mshiriki kutoa elimu kwa wananchi wenu kwa kushirikiana na watendaji ili walengwa wanunue vitambulisho hivyo , kwani fomu ni bure na kitambulisho ni Sh 20,000” Ameongeza DC Chonjo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Sheilla Lukuba,amewaomba Watendaji wa Kata kushiriki kikamilifu kuhamasisha na kutoa elimu kwa walengwa ili waweze kuwa na vitambulisho hivyo kwa kuwa suala hilo litawasaidia kuwaondolea usumbufu wakati wa kufanya biashara zao.
"Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, amevitoa Vitambulisho hivi kwa njia njema ili wafanyabiashara ndogondogo wasinyanyaswe na kufanya kazi zao kwa Uhuru nchi nzima bila kusumbuliwa na mtu yeyote, jukumu letu ni kutekeleza kwa kuvinunua ili viendelee kutusaidia hii ni fursa ambayo Mhe Rais wetu Dkt John Magufuli ametupatia, jukumu letu ni kutekeleza kwa vitendo, miaka ya nyuma kamatakamata ya migambo ilikuwa kubwa hata biashara zenu zilikuwa za shida lakini leo mpo huru kwa Bei ya 20,000/= tulipe Kodi kwa maendeleo ya Taifa letu"Amesema Lukuba.
"Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, amevitoa Vitambulisho hivi kwa njia njema ili wafanyabiashara ndogondogo wasinyanyaswe na kufanya kazi zao kwa Uhuru nchi nzima bila kusumbuliwa na mtu yeyote, jukumu letu ni kutekeleza kwa kuvinunua ili viendelee kutusaidia hii ni fursa ambayo Mhe Rais wetu Dkt John Magufuli ametupatia, jukumu letu ni kutekeleza kwa vitendo, miaka ya nyuma kamatakamata ya migambo ilikuwa kubwa hata biashara zenu zilikuwa za shida lakini leo mpo huru kwa Bei ya 20,000/= tulipe Kodi kwa maendeleo ya Taifa letu"Amesema Lukuba.
Zoezi hili la Vitambulisho vya Wajasiriamali linatekelezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na Mamlaka
ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na Idara ya Uhamiaji.
Post a Comment