DC MSULWA AFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI JIMBO LA MOROGORO MJINI .
Mbunge wa jimbo la Morogoro Mjini Mhe. Abdulaziz Abood.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa,
amefurahishwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM Jimbo la
Morogoro Mjini iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Abdulaziz
Abood.
Kauli hiyo ya kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi
CCM Jimbo la Morogoro Mjini, ameitoa leo wakati wa makabidhiano ya Ofisi na
aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mstaafu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo leo Juni 25, 2020 katika
Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na
Waandishi wa habari, amesema licha ya ugeni wake katika Wilaya ya Morogoro
lakini amekuwa akimfahamu Mhe. Abood kwa muda mraefu jinsi anavyowatumikia
Wananchi wa Jimbo lake pamoja na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili
wananchi wake.
Aidha, amewataka Watumishi kuichukua Ilani hiyo ya Utekelezaji wa Jimbo la Morogoro Mjini kuisoma ili kujua ni yapi yamefanyika katika kipindi cha miaka 5 chini ya Uongozi wake wa Ubunge kwa maslahi ya Wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
"Niendelee kumpongeza sana Mhe. Abood kwa kazi alizozifanya katika kipindi chote cha miaka mitano cha Ubunge wake na kwamba ripoti ambayo amenikabidhi nitaisoma ili niweze kuona jinsi ya shughuli mbali mbali alizozifanya na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ilivyofanyika" Ameongeza DC Msulwa.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Morogoro , Mhe. Abdulaziz Abood, amesema yapo mengi yamefanyika lakini kwa sababu huu sio muda wa kufanya kampeni muda ukifika atayazungumza yale yaliyofanyika katika kipindi hiki cha miaka mitano tangia mwaka 2015 hadi 2020.
""Namshukuru sana Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli, kwakweli amekuwa akijitoa sana kwa wananchi hata hii miradi mikubwa mnayoiona ikiendelea katika Manispaa yetu ya Morogoro ni maono yake ya kutaka wana Morogoro tuishi vizuri na kupata fursa mbalimbali za kibiashara, lakini kwa kunipa miradi mikubwa kama hii nampongeza sana , kwa upande wetu wa Morogoro ameshapita tayari kikubwa tunasubiri kuapishwa ili azidi kusongesha Taifa hili mbele ili kufikia uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda" Amesema Mhe. Abood.
Mhe. Abood, amesema ataendelea kushirikiana bega kwa bega na serikali katika miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ile ya kimikakati pamoja na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi.
Aidha amesema kuwa katika kipindi chote cha Uongozi wake wa miaka mitano chini ya Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli aliweza kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo pamoja na kutatua changamoto mbali mbali ambazo zilikuwa zinawakabili wananchi wa maeneo mbali mbali ya Jimbo la Morogoro Mjini.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wake aliweza kuweka mipango madhubuti katika masuala ya kuleta maendeleo katika Nyanja mbali mbali zikiwemo sekta ya afya, elimu, nishati ya umeme pamoja na kutoa elimu kwa wananchi katika mambo mbali mbali ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse,amempongeza Mhe. Abood kwa kuweza kushirikiana bega kwa bega na serikali ya awamu ya tano katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo na miradi mbali mbali ya kimikakati kama vile Soko Kuu la kisasa pamoja na Stendi Mpya ya Daladala.
“Mimi kama Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, nampongeza sana Mbunge wetu Mhe. Abood kwa kuweza kushirikiana naye kwenye mambo mbalimbali kwa kweli ameonyesha uzalendo mkubwa na huu ni mfano mzuri wa kuigwa kwa wabunge wengine, tuna mengi katufanyia , ukiangalia sasa tuna Ambulence Mpya ya kisasa ya kubebea wagonjwa hii ni nguvu yake Mhe. Abood kwakweli tuna kila sababu ya kumpongeza ""Amesema Waluse.
Ikumbukwe kuwa Ilani aliyoikabidhi Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro imebainisha kazi mbali mbali ambazo amezitekeleza katika jamii katika kipindi chake cha miaka mitano (5) ikiwemo katika sekta ya afya, elimu,nishati ya umeme pamoja na kutatua changamoto za wananchi.
Post a Comment