UZINDUZI WA BARAZA LA WAZEE KILAKALA, DIWANI KANGA, ATOA NENO LA MATUMAINI KWA WAZEE.
DIWANI wa Kata ya Mhe. Marco Kanga, amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma kwa Wazee hususani Wazee wa Kata ya Kilakala.
Kauli hiyo ameisema leo Aprili 03/2022 katika sherehe za uzinduzi wa Baraza la Wazee Kata ya Kilakala lililofanyika katika Shule ya Sekondari Kingalu.
Akizungumza na Wazee waliojitokeza katika uzinduzi huo wa Baraza la Wazee, Mhe. Kanga, amesema kuwa Serikali inatambua kuwa wazee ni hazina katika kuibua na kuchochea shughuli mbalimbali za kimaendeleo kutokana na ushauri mzuri wanaotoa wanaposhirikishwa katika mambo ya kimaendeleo.
"Serikali itaendelea kujiimarisha katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa Wazee kwa kuzingatia umuhimu wa kundi hili katika jamii yetu , Manispaa yetu ya Morogoro kwa kuwatambua Wazee wameanza kutatua changamoto ya vitambulisho vya msamaha wa matibabu bure kwa wazee wetu , hii ni hatua kubwa ambayo Manispaa yetu imeifanya, kwahiyo tuweni na subra zoezi hili bado lipo na litaendelea kuwepo "Amesema Mhe.Kanga.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kanga, amesema Serikali itahakikisha kwamba wanaenda kutatua changamoto za haraka kwa Wazee kupata stahiki zao mapema pindi wanapo staafu kazi ili waweze kujikimu wakiwa nyumbani.
Kanga, amewahimiza wazee kuwa na utaratibu wa kwenda kucheki afya zao mara kwa mara ili kupata huduma stahiki kwa wakati kwani huduma za afya kwa wazee kuanzia miaka 60 ni bure katika vituo vyote vya kutolea huduma.
Kupitia Uzinduzi huo wa Baraza la Wazee, Kanga, ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wazee hao juu ya UVIKO-19 na kuwataka wazee kuendelea kuchanja, kwani wapo kwenye kundi ambalo ni rahisi kupata maambukizi hayo huku akiwatoa hofu kwamba chanjo hii ni salama kabisa na kuwataka kumuunga mkono Mhe.Rais alieona umuhimu wa kuokoa maisha ya watanzania kwa kupata chanjo hii.
Kwakumalizia , Mhe. Kanga , ameishukuru serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali wazee na kuwaandalia mazingira mazuri ya kupata huduma za afya na kuwapunguzia ukali wa maisha kupitia mfuko wa TASAF.
Post a Comment