Header Ads

DIWANI BUTABILE AWAPA NENO WAHITIMU KIDATO CHA SITA SEKONDARI MAFIGA.

WAHITIMU wa kidato cha sita Shule ya Sekondari Mafiga Manispaa ya Morogoro, wametakiwa kusoma kwa bidii ili waweze kuitumikia nchi yao kwa uzalendo katika fani mbalimbali baadaye.

Ushauri huo umetolewa leo Aprili 1/2022 na Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, akiwa mgeni mwalikwa  kwenye mahafali ya  tano (5) ya Kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Mafiga.

Aidha, Mhe. Butabile, amewataka wanafunzi hao kujifunza uzalendo na uaminifu kwa nchi yao ili watakapopata kazi mara baada ya kumaliza shule waiwezeshe nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kasi.

Licha ya kuzungumzia uzalendo, amesema  ili taifa liweze kusonga mbele kwa kasi kiuchumi linapaswa kuwa na wasomi waliobobea kwenye taaluma mbalimbali badala ya kutegemea wataalamu kutoka mataifa mengine.

“Mnapaswa kujiandaa vya kutosha kwasababu taifa linawategemea mje kuilitumika kwenye fani mbalimbali hivyo hakikisheni mnafaulu kwa viwango vya juu sana,” Amesema Butabile.

Aidha, ameupongeza uongozi wa shule na wanafunzi wa shule hiyo kwani takwimu zinaonyesha kuwa imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma mwaka hadi mwaka na amewataka wasibweteke na mafanikio hayo.

“Mmekuwa mkifanya vizuri nawaomba muendelee kufanya vizuri zaidi na ikiwezekana muwe kwenye 10 bora kitaifa mwaka huu na naamini mkiweka nia mtafanikiwa kufika kwenye kumi bora,” Ameongeza Butabile.

Shule ya Sekondari Mafiga ni miongoni mwa shule kongwe za sekondari zilizopo Manispaa ya Morogoro ambapo kwa mwaka huu jumla ya wahitimu 108 wanakwenda kufanya mtihani wa Taifa kuanzia tarehe 9/5/2022  ikiwamo Wavulana 58 na wasichana 50.

Mwisho, ameiomba Serikali kuweka uzio katika shule hiyo kwa ajili ya ulizni na usalama wa wanafunzi ikiwamo kujengewa Hosteli ili wanafunzi waweze kukaa shuleni hususani Mabinti katika kuepuka vitendo vya ushawishi.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.