DIWANI CHOMOKA AKABIDHI MILIONI 5 JUKWAA LA WANAWAKE MKUNDI, ATOA NENO ZITO JUU YA MIRADI WANAYOIFANYA.
WANAWAKE wajasiriamali Kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro wametakiwa kubuni miradi yenye tija na mwelekeo wa viwanda ili waweze kujiongezea tija katika uzalishaji na kuongeza wigo wa ajira kwa jamii inayowazunguka.
Hayo yamesemwa Aprili 02/2022 na Diwani wa Kata ya Mkundi, Mhe. Seif Chomoka, katika Kongamano la Wanawake Kata ya Mkundi lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo Cha Uandishi wa Habari MSJ.
Akizungumza na Wanawake waliojitokeza katika Kongamano hilo, Mhe. Chomoka, amesema vikundi vingi vya wanawake havipo katika mrengo wa viwanda vidogo vidogo jambo linalowakosesha wanawake mapato huku akiwakumbusha kuendelea kuwatumia wataalamu waliopo ngazi ya Halmashauri ili kujiongezea ujuzi na wigo wa ufanyaji wa biashara.
"Leo nimefurahi kukutana na nyinyi, hii pesa milioni 5 ninayoitoa leo ni kwa ajili ya kuwasaidia muweze kukopeshana mkiachilia mbali mkopo wa Manispaa, nataka kuona miradi yenye tija, hamisheni akili zenu katika miradi yenye tija ili muweze kujiongezea vipato, mnao wataalamu wa Manispaa shirikianeni muone jinsi mtakavyoweza kupiga hatua kubwa zaidi nayi muweze kujikimu katika kusaidia familia zenu" Amesema Mhe. Chomoka.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Moro Batiki, Dkt. Herrieth Mkaanga, amesema asilimia kubwa ya wanawake wameondokana na dhana ambazo zilikuwa zikiwafunga na kushindwa kujikita katika shughuli za kimaendeleo huku akisema masuala ya usawa wa haki kwa wanawake yamekuwa ni kipaumbele katika jamii kwa sasa.
Katika hatua nyengine, Mhe. Chomoka amesema asilimia kubwa ya miradi imeshatengewa fedha na ipo katika hatua za utekelezaji , ambapo miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo maji pamoja na barabara inaendelea kutekelezwa huku akiwakumbusha kuendelea kuiamini serikali kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayowagusa wananchi.
Post a Comment