Header Ads

KAMATI YA FEDHA NA UTAWALA MANISPAA YA MOROGORO ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO.


KAMATI  ya Fedha na Utawala  Manispaa ya Morogoro, imeridhishwa na kupongeza hatua ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Hayo yamejiri leo Aprili 20/2022 wakati ikifanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo mradi wa Zahanati ya Tungi ambayo Manispaa inapendekeza kuitanua na kuibadilisha kuwa Kituo cha Afya, Soko la Mwanzo Mgumu Kata ya Mwembesongo,Ujenzi wa Madarasa Shule ya Msingi Kilakala kufuatia baadhi ya madarasa kuangukiwa na mti na kuleta uharibifu mkubwa,  Shule mpya ya Ghorofa iliyopo Kata ya Boma, pamoja na Mabanda 3 ya Machinga yaliyopo maeneo ya Fire Sabasaba.

Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu, Mhe. Pascal Kihanga, walijionea hatua za ujenzi wa Shule mpya ya Ghorofa yenye madarasa 15 iliyopo Kata ya Boma ambapo kwa sasa ujenzi huo umefikia asilimia 29, Zahanati ya Tungi,Soko la Mwanzo Mgumu Kata ya Mwembesongo, Ujenzi wa Madarasa Shule ya Msingi Kilakala, pamoja na Mabanda 3 ya Machinga yaliyopo maeneo ya Fire Sabasaba.

Wakizungumza kuhusu ujenzi wa Vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Kilakala, wajumbe wamesema 

Kukamilika kwa miundombinu hiyo ya kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo kufuatia baadhi ya madarasa kuangukiwa na mti na kuleta uharibifu mkubwa  na hivyo kutekeleza kwa ufanisi sera ya elimu bila malipo.

Kuhusu Soko la Mwanzo Mgumu, Mstahiki Meya ,amesema wanajipanga kuhakikisha eneo ambalo wafanyabiashara wanauza sasa kujengwa Mabanda kama yalivyo ya Fire hivyo kwa sasa wafanyabiashara hao wanatakiwa kuingia Soko Jipya ambalo lina mandhari mazuri ya kufanyia biashara zao na usalama wa walaji.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mhe. Ally Kalungwana, amesema watahakikisha kuwa Soko la Mwanzo Mgumu linakuwa Soko lenye tija kwani hawapo kwa ajili ya kuwanyanyasa wafanyabiashara bali wanataka kuona wafanyabiashara hao wanafanya biashara katika mazingira rafiki.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema Soko la Fire baada ya wiki mbili linaweza kukamilika na wafanyabiashara kuanza kufanya kazi baada ya uzinduzi wa Soko hilo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.