RC MOROGORO AZINDUA RASMI MICHEZO YA MEI MOSI, ATOA NENO.
MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amezindua rasmi michezo ya Mei Mosi ikiwa ni maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kitaifa itafanyika Mkoani Morogoro.
Wakati wa uzinduzi huo Mhe. Fatma Mwassa amewataka Wakuu wa Taasisi za Serikali na Waajiri wa sekta nyingine hapa nchini, kuwaruhusu Wafanyakazi wao kushiriki michezo hiyo pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya maadhimisho ya Mei Mosi ijayo.
Fatma Mwassa ametoa Ushauri huo leo Aprili 20 mwaka huu wakati wa uzinduzi huo ambapo pia amekagua timu mbalimbali za michezo tayari kwa kuanza mashindano hayo ambayo yanafanyika uwanja wa Jamhuri uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya Wakuu wa Taasisi na Waajiri kutowaruhusu watumishi wao kushiriki michezo wakati wa maadhimisho hayo kwa kisingizio cha ukosefu wa fedha, hivyo amewaomba waajiri wote pamoja na Taasisi za Serikali kutoa msukumo kwenye suala la michezo kwa kuwa michezo inajenga Afya, utimamu wa mwili, kuongeza tija kazini na kuimarisha mahusiano baina ya wafanyakazi.
“...naomba kuwakumbusha Viongozi watenge bajeti kwa ajili ya michezo na pia watenge muda kwa wafanyakazi wao kufanya michezo, kwa kufanya hivyo wafanyakazi watakuwa na utimamu wa mwili na kuongeza tija kazini...” amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Maadhimisho ya Mei Mosi huambatana na michezo mbalimbali kwa lengo la kuonesha umuhimu wa wafanyakazi kuwa pamoja na kuimarisha Afya za Wafanyakazi.
Kwa upande wao washiriki wa michezo hiyo akiwemo Kocha wa timu ya kuvuta kamba kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Bw. Nikasi Luanda amesema wamekuja kutetea ubingwa wao kwenye mashindao haya kwa kuwa mashindano yaliyopita ambayo yalifanyika Mkoani Dodoma waliibuka washindi wa kwanza kwa upande wa Wanawake na Wanaume na wanaamini mwaka huu pia watakuwa mabingwa kwa michezo hiyo.
Kilele cha Maadhimisho ya Mei Mosi Kitaifa mwaka huu yatafanyika Mkoani Morogoro katika uwanja wa Jamhuri, Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli mbiu ya Mei Mosi mwaka huu ni “Maslahi Bora, Mishahara juu, kazi iendelee” wakati kaulimbiu ya Michezo ya Mei Mosi inasema “Miaka miwili ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeimarisha michezo na kuongeza ufanisi kazini, Kazi iendelee”.
Post a Comment