Header Ads

MKURUGENZI IDARA MICHEZO WIZARA YA ELIMU ZANZIBAR AAHIDI MAZITO SHULE YA GREEN APPLE


MKURUGENZI Idara ya Michezo na Utamaduni kutoka Wizara ya Elimu Zanzibar , Ahmed Abdallah Mussa, ameahidi mambo makubwa shule ya Green Apple iliyopo Manispaa ya Morogoro akiwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 6  Darasa la awali (chekechea)   yaliyofanyika hivi karibuni mwishoni mwa Novemba 2023.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mussa ,amesema kuwa moja ya vitu ambavyo ameahidi ni kutoa mafunzo ya kozi fupi ya wiki moja  kwa mkutubi wa Shule ya Green apple ili kusaidia katika uendeshaji bora wa maktaba ya shule inayotarajiwa kufunguliwa mwaka 2024  , vifaa vya michezo , tofali 300 kwa jili ya kuchangia ujenzi wa  uzio pamoja na kuwaalika walimu wa Green Apple kutembea Zanzibar kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na waalimu wa Zanzibar pamoja na mapumziko mafupi ya waalimu hao kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Zanzibar.

Mussa, amesema amefurahishwa na taaluma katika shule hiyo huku akiwataka wazazi kutengeneza urafiki wa karibu na waalimu wa watoto ili wawe wanapata mrejesho wa kinachoendelea badala ya kuwaacha tu baada ya kulipa ada.

"Jukumu la taaluma tusiwaachie waalimu peke yao, sisi wazazi tunapaswa kuwa mstari wa mbele kufuatilia mienendo ya watoto wetu shuleni, elimu ni pembe tatu, waalimu, wanafunzi na wazazi kama kweli tunataka watoto wetu wafaulu vizuri , lakini tusiwaache mbali kwenye michezo nimeona watoto wana vipaji naomba wazazi kwa kushirikiana na waalimu endelezeni vipaji vyao " Amesema Mussa.

Aidha,Mussa, amefurahishwa sana na igizo lililofanywa na watoto hao juu ya mabadiliko ya tabianchi ,ikiwa ni pamoja na umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwasihi wazazi kuwa na tabia ya upandaji miti ili kuunga mkono juhudi za Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

Mwisho,ameipongeza shule hiyo kwa maendeleo yake ya kitaaluma na kuwataka wasibweteke na mafanikio wanayoyapata bali waendelee kuhakikisha wanafunzi wao wanafaulu kwa alama za juu.

Naye Mkurugenzi wa Shule ya Green Apple, Mwajabu Dhahabu, amesema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2017 , shule imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma japo kwa mwakani itazalisha darasa la saba kwa mara ya kwanza lakini wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri sana katika mitihani ya darasa la nne.

"Mfano mwaka 2022 wanafunzi wa darasa la nne wote walipata ufaulu wa alama A ,niwatoe hofu wazazi juu ya taaluma inayotolewa  shuleni hapa ni ya uhakika na inayofuata mtaala wa wizara ya elimu" Ameongeza Mwajabu.

Amesema Green apple, ni miongoni mwa shule zinazofanya vizuri kitaaluma kwani ina madarasa ya kutosha ili kuhakikisha mwalimu anakuwa na uwezo wa kumfikia kila mwanafunzi wake.

"Mbinu pekee ya ufaulu katika shule yetu ya Green apple Pre & Primary ni kuwa na madarsa ya kutosha lakini kuwa na waalimu mahiri na wabobezi wa kutosha kwa masomo wanayofundisha hali ambayo imewawezesha wanafunzi kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya Kitaifa kwa upande wa darasa la 4 ambapo mwakani tunatarajia kuwa na darasa la 7 ambapo imani yetu pia watafanya vizuri Kitaifa  " Amesema Mwajabu.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.