LUKWELE AWATWISHA WAZEE JUKUMU LA MALEZI NA MAADILI
NAIBU Meya wa Manispaa ya Morogoro akimwakilisha Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Mohamed Lukwele, amewataka Wazee kuwa chachu ya malezi na maadili ili kurudisha maadili ambayo yamepotea kwa Jamii.
Hayo ameyazungumza Desemba 20/2023 katika uzinduzi wa Kamati ya Maadili ya Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro kwenye Ukumbi wa Soko Kuu la Chifu Kingalu.
Mhe. Lukwele, kutokana na mmomonyoko wa maadili ulioshamiri kwa sasa Wazee kupitia kamati ya maadili wana nafasi kubwa kukemea vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya jamii ya kitanzania.
"Sasa hivi tunapita kwenye kipindi cha mmomonyoko wa maadili, kwani umeenea ndani ya jamii nyingi, ni changamoto sana na sisi kama Wazee kupitia kamati yenu ya maadili tusimame vizuri, tusiposimama vizuri kwa nafasi yetu kubeba ulezi wa jamii tunaweza tukajikuta tunapata Wazee wa kesho na keshokutwa ambao watashindwa kulea vizazi vinavyokuja" Amesema Mhe. Lukwele.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Morogoro, Samwel Mpeka, amesema ni wakati sasa wa Kamati ya Maadili kibebe jukumu la kujua kinafanya nini ili maadili ya vijana yaendelee kuwa mazuri kwa manufaa ya kizazi kijacho.
"Katika zama hizi tunahitaji zaidi Wazee waendelee kufanya mengi ili kuambukiza vizazi vipya tabia njema na kuwezesha nao kufikia uzee ulio mwema lakini cha kusikitisha hivi karibuni kumekuwa na Wazee wanaoripotiwa kufanya matukio ya ajabu yasiyolingana na umri wao mfano kubaka na kulawiti watoto, kuwaoza watoto wadogo na kupandikiza imani mbaya, tukemee haya matendo tuwe mstari wa mbele kuhakikisha maadili yanakuepo " Amesema Mpeka.
Naye Diwani wa Kata ya Kihonda, Mhe. Hamis Kilongo , ameiomba Kamati ya maadili kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kutekeleza afua mbalimbali kwa ustawi wa Wazee.
Kwa upande wa Afisa Ustawi Manispaa ya Morogoro, Sidna Mathias , amesema Serikali imekuwa ikichukua za kuhakikisha Ustawi wa Wazee ikiwemo kuimarisha mifumo ili wazee wapate huduma za kijamii kama Afya, ulinzi, usalama na matunzo kwenye makazi ya wazee, kupitia upya Sera ya Wazee na kuanzisha mabaraza ya wazee.
Katibu wa Wazee Manispaa ya Morogoro, Bakili Anga, amesema Baraza la wazee limekuwa likikabiliwa na changamoto kama usafiri, maji kweye ziara zao, sehemu ya kufanya vikao, sare za kamati za Maadili, vipaza sauti ,vitendea kazi na bima ya afya kwa wazee.
Dr. Anga, amesema lengo la Baraza la wazee ni kuwasaidia Wazee katika masuala mbalimbali ikiwemo matibabu kupitia bima ya Afya na kudumisha maadili mema kwa jamii.
Miongoni mwa waliohudhuria Baraza hilo ni Diwani wa Kata ya Mzinga, Mhe. Salum Chunga, Diwani wa Chamwino Mhe. Abdallah Meya, Diwani wa Kata ya Kihonda, Mhe. Hamisi Kilongo, Zuia Traffic, Itra, mwakilishi wa Mzinga, Mkurugenzi wa Shirika la kusaidia Wazee MOREPEO , Samson Msemembo na wataalamu kutoka Ofisi ya Manispaa ya Morogoro.
Post a Comment