MICHEZO YAZIKUTANISHA MANISPAA YA MOROGORO, MORO DC KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIKA 62 YA UHURU WA TANZANIA BARA.
KUELEKEA Maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, watumishi wa Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro wameshiriki michezo mbalimbali sambamba na uandishi wa Insha kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari.
Michezo hiyo imefanyika Disemba 8,2023 katika Kiwanja cha Mpira shule ya Msingi Mwere iliyopo Kata ya Kingo ikijumuisha michezo ya mpira wa Miguu , Netball na kuvuta kamba.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa michezo hiyo, Afisa Tawala Wilaya ya Morogoro akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Ndg. Hilary Sagara, amesema kuwa michezo ni afya hivyo kuelekea miaka 62 ya Uhuru muhimu kuimarisha afya ili kuendelea kuleta maendeleo.
“Michezo ni afya hivyo kuelekea katika maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa wa Tanzania Bara tumeona ni vyema tukawa na michezo ,kwanza inakutanisha jamii, kubadilishana ubunifu wa kiutendaji lakini michezo inaimarisha afya zetu lakini pia upande wa Insha, tutakwenda kuwatangaza washindi waliofanya vizuri katika uandishi wa insha ambazo zinazungumzia miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara kwa upande wa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari" Amesema Sagara.
Katika upande wa Insha,, amesema wanafunzi wote wamewasilisha insha zao na kusikilizwa na kamati maalum ambapo wanafunzi watakaoibuka washindi watakabidhiwa zawadi zao katika Madahalo wa maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru utakaofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Disemba 9,2023.
Katika hatua nyengine, Sagara,amesema mwakani watahakikisha kunakuwa na michezo mingi zaidi ya hii ambayo imefanyika kwani zipo changamoto walizoziona na watazifanyia kazi katika maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru ya mwakani 2024.
Naye, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewapongeza wanamichezo walioshiriki katika michezo mbalimbali huku akiwaalika wananchi kushiriki katika
Mdahalo wa miaka 62 ya uhuru utakaofanyika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Disemba 9,2023.Katika michezo hiyo, Timu ya mpira wa miguu ya Manispaa ya Morogoro iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya timu ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro , upande wa Netball Manispaa walishinda 75-2 dhidi ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na upande wa kuvuta kamba Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ilishinda dhidi ya timu ya Manispaa ya Morogoro.
Post a Comment