Header Ads

MD MACHELA ALIVALIA NJUGA SUALA LA MRUNDIKANO WA TAKA MITAANI.

MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela,amefanya ziara ya kukagua maeneo ambayo yanachangamoto ya mrundikano wa takataka katika Mitaa pamoja na kupokea maoni ya wananchi.

Ziara hiyo imefanyika Desemba 08/2023 katika Kata 2 ikiwemo Kata ya Mwembesongo na Mafiga akiambatana na Afisa usafishaji na udhibiti wa taka ngumu Manispaa ya Morogoro, Samwel Subi pamoja na Viongozi wa Kata na Mitaa.

Akizungumza na wananchi katika ziara hiyo, MD Machela, amesema lengo la ziara ni kupokea maoni ya wananchi juu ya mrundikano wa taka na kuangalia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto za taka ili kuona namna ya kufanya usamabazaji wa magari na hatua madhubuti ya kufikisha taka dampo.

Hata hivyo, MD Machela, baada ya kuona taka hizo amewataka Watendaji kuzidi kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili taka hizo zisiendelee kuwa mitaani na kusababisha magonjwa.

Machela, amesema Manispaa ya Morogoro  licha ya uwepo wa vifaa maalumu kwa ajili ya kutunzia taka   (backet)  yapo pia magari ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubeba taka  hizo ambapo kwa sasa amesema magari yote yanafanya kazi na watayapanga kwa utaratibu maalumu ili yahudumie wananchi .

Aidha, amesema malengo ya Manispaa ni kuwa miongoni mwa miji safi nchini hivyo kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na ushirikiano wa viongozi ,watendaji na wananchi na mbinu mbalimbali atahakikisha suala la taka mitaani linapatiwa ufumbuzi wa kina.

"Taka bado zipo mtaani nimejionea kwa macho nimefanya ziara yangu hii nikiwa na afisa usafishaji na udhibiti wa taka ngumu Manispaa ya Morogoro , mpango wetu tunakwenda kukaa chini na Watendaji wa Kata, Mitaa , Wenyeviti wa Mitaa na wawakilishi wa wananchi kuona mikakati gani ambayo tutakubaliana kwa pamoja kuhakikisha adha ya mrundikano wa taka mitaani unapatiwa suluhu, Jumatatu tarehe 11/12/2023 tutaanza Kata ya Mwembesongo na kuendelea na Kata nyengine kupata muarubaini wa taka kurundikana mitaani" Amesema Machela.

Pia, Machela, amewataka wananchi kuchukua jitihada za makusudi kufikisha taka maeneo ambayo yametengwa ili kuepusha magonjwa ya  mlipuko ikiwemo  kipindupindu.

Naye, Afisa usafishaji na udhibiti wa taka ngumu, Samwel Subi, ameataka wananchi kuendelea kulipa ada ya usafi kwani taka haziewezi kufika dampo kama wananchi watasua sua kulipa ada.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.