MANISPAA YAFANYA MDAHALO KUADHIMISHA MIAKA 62 YA UHURU
MKUU wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa, Desemba 9,2023 ameshiriki kwenye mdahalo kujadili maendeleo mbalimbali yaliyopo katika Wilaya ya Morogoro tangu kupatikana kwa Uhuru wa Nchi yetu hadi sasa.
Mdahalo huo umefanyika katika ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni Siku ya Maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Maadhimishp hayo, yalitanguliwa na matukio mbalimbali wakati wa juma la kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Uhuru, matukio hayo ni pamoja na zoezi la upandaji miti, mashindano ya Insha, usafi wa mazingira na shughuli za Kijamii, bonanza la michezo pamoja na mahojiano maalum na wazee huku maadhimisho hayo yakibeba kaulimbiu isemayo “Miaka 62 ya Uhuru, Umoja ni mshikamano, ni chachu ya Maendeleo ya Taifa letu"
DC Nsemwa, amesema katika miaka 62 ya uhuru Wilaya ya Morogoro imefikia maendeleo makubwa sana ukiangalia Sekta ya elimu kwa sasa kila Kata ina shule za Kata ambapo amesema yote hayo ni matunda ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza Sekta ya elimu nchini.
Aidha, DC Nsemwa, ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia kwa kuipatia Wilaya ya Morogoro fedha za miradi ya Maendeleo ikiwemo miradi ya maji, Shule, madarasa , miundombinu na na umeme.
Katika mdahalo huo mada mbalimbali zimewasilishwa kama vile kuhusu Elimu kutoka Uhuru hadi sasa, Siasa toka uhuru hadi sasa, uchumi na maendeleo kutoka Uhuru hadi sasa pamoja na kutathmini maendeleo katika miaka 62 ya uhuru wa Tanzania bara.
Akiwasilisha mada ya siasa na maendeleo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga,amewataka wananchi kuendelea kuenzi maneno ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku akitoa salamu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia Manispaa ya Morogoro fedha nyingi kwenye Sekta ya elimu pamoja na Sekta ya afya.
Kwa upande wa Katibu wa kwanza wa TANU 1958 Wilaya ya Morogoro , Mzee Juma Salum Digallu, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha siasa safi toka kipindi tunapata Uhuru tukiwa na chama kimoja hadi sasa Tanzania imekuwa na vyama vingi vya siasa vilivyosajiliwa kwa kudumu jambo ambalo ni ishara yakuwa na siasa safi inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwepo pia kuwatoa wanasiasa walioko magerezani kurudi uraiani na kufanya siasa.
Naye , Mwenyekiti wa Mdahalo wa miaka 62 ya uhuru, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya Mstaafu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amesema kabla ya uhuru Tanzania hakukuwa na Chuo Kikuu bali vyuo vilianza kupatikana kwa kuchangia kutoka kwa wananchi lakini sasa Tanzania imebadilika na Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa pesa nyingi kujenga madarasa kuendeleza elimu.
Aidha, Mhe. Msulwa, amesema katika msingi ya uongozi bora ni uaminifu na uzalendo wa kweli kwa kujali maslahi ya Nchi na ukiwa mzalendo utekelezaji wa siasa safi utafanyika na rushwa haitakuwepo huku akiwataka Wananchi kuenzi mambo yote kutoka wakati wa uhuru hadi leo kwa kusimamia yale mazuri na kuwa wazalendo wa kweli kwa maslahi mapana ya Nchi.
Katika mdahalo huo ,ulienda sambamba na utoaji wa zawadi za washindi wa bonaza la michezo mbalimbali iliyofanyika Desemba 8/2023 ikiwa ni wiki ya maadhimisho ,ambapo upande wa mpira wa miguu , Manispaa ya Morogoro waliibuka kinara kwa kuifunga Moro DC mabao 2-1, upande wa kuvuta kamba Moro Dc walikuwa washindi dhidi ya Manispaa, na upande wa Netball Manispaa walishinda 75-2 dhidi ya Moro DC , uandishi wa insha Samia Ibrahimu mwanafunzi wa darasa la 6 Shule ya Msingi Mafiga B alishinda na upande wa Sekondari, Gloria Erick kidato cha 5 HKL Shule ya Sekondari Mafiga alishinda uandishi wa insha.
Post a Comment