MANISPAA YAKUTANISHA WADAU WA MAENDELEO KUJADILI MIRADI YA KIMKAKATI INAYOTARAJIWA KUANDIKIWA MAANDIKO
MANISPAA ya Morogoro imewakutanisha wadau wa maendeleo na wataalamu wa Manispaa katika kikao chenye lengo la kujadili, kutoa maoni na ushauri juu ya namna bora ya kuboresha miundombinu ya kimkakati inayotarajiwa kuandikiwa Maandiko na Manispaa ya Morogoro.
Kikao hicho cha wadau kimefanyika Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa ya Morogoro Desemba 22/2023 kikihudhuriwa na wadau wa maendeleo pamoja na wataalamu wa Manispaa
Akizungumza mara baada ya kufungua kikao hicho, Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga, amewataka wadau wa maendeleo kuhakikisha wanaibua hoja zenye tija zitakazoleta msingi wa kuboresha na kulinda miundombinu ya miradi ya Kimkakati itakayosaidia kuinua uchumi wa nchi na kuongeza mapato ya Manispaa.
"Tumewaita hapa wadau ili kuomba mawazo na mitazamo yenu chanya juu ya kuiendeleza Manispaa yetu na kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi" Amesema Mhe. Kihanga.
Naye Mwakilishi wa Katibu Tawawala wa Wilaya ya Morogoro, Hilary Sagara, ameipongeza Manispaa kwa kuwaalika wadau wa maendeleo kujadili maendeleo ya Manispaa yao ili kuwa na tija katika miradi wanayopendekeza kuiandikia maandiko kwa ustawi wa maendeleo ya Manispaa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Machela, lengo la kuandika miradi ya maandiko ya kimkakati ni kutafuta fedha ili kujenga miundombinu ambayo itakuwa ni kichocheo cha maendeleo ya Manispaa ya Morogoro kwa kuongeza mapato ya ndani ,kutoa ajira , kupendezesha mji, kipato kwa wana Manispaa na kuboresha huduma za kijamii.
Machela,amesema Manispaa imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za kiuchumi ili kukidhi vigezo vya kuwa Jiji hivyo mawazo chanya ya wadau yataiwezesha Timu ya Maandiko na Menejimenti kuandaa maandiko ya kimkakati ambayo yataweza kutekelezeka kikamilifu.
Miongoni mwa mapendekezo ya miradi ya kimkakati iliyopewa kipaumbele ni ujenzi wa machinjio ya kisasa Mkundi,ujenzi wa majengo ya kibiashara (Mwembesongo), ujenzi kituo cha maegesho ya malori na ghala Kihonda,ujenzi wa jengo la kibiashara (Shopping Mall na Hotel Msamvu), ujenzi wa Soko la Kisasa Manzese, ujenzi wa soko la kisasa la machinga Nanenane, ujenzi Kituo cha maegesho ya malori nanenane,mipango ya Housing Estates katika maeneo ya Forest na Boma Road ,ujenzi wa Hotel ya nyota 3 Kihonda, Ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa watu 600 wenye jiko la kisasa, kumbi 2 ndogondogo za watu 200-100 ,ujenzi wa ghala na ujenzi wa Uwanja wa Michezo Kihonda.
Post a Comment