DIWANI KANGA AKABIDHI MKOPO WA BAJAJI KWA MWANANCHI MWENYE ULEMAVU WA MGUU.
Diwani wa Kata ya Kilakala Mhe. Marco Kanga,(kushoto) akimkabidhi Bajaji Ndg. Frank Sanga (kulia).
Frank Sanga, akizungumza na kutoa shukrani mara baada ya kukabidhiwa Bajaji hiyo.
Bajaji aliyokabidhiwa Frank Sanga.
DIWANI wa Kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro , Mhe. Marco Kanga, amekabidhi Mkopo wa Bajaji moja unaotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa, Frank Sanga , mwenye ulemavu wa mguu Mkazi wa Mtaa wa Kigurunyembe Kata ya Kilakala.
Tukio hilo la kukabidhiwa Bajaji limefanyika hivi mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka 2022 katika Ofisi ya Kata ya Kilakala.
Akizungumza mara baada ya kumkabidhi Bajaji hiyo, Mhe. Kanga, amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuwajali na kuwasaidia watu wenye ulemavu ili waweze kujikwamua na kujikomboa na maisha na kukuza uchumi binafsi na familia zao.
Kanga, amesema Serikali inathamini uwepo wa watu wenye ulemavu na tayari Halmashauri imetimiza wajibu wake kwa kutoa mkopo na ameitaka jamii na Wananchi kwa ujumla kuwaibua watu wenye ulemavu walioko majumbani.
Aidha, Mhe. Kanga, amemtaka kijana huyo aliyepatiwa Mkopo wa Bajaji kuendelea kupambana na maisha kwa kutumia chombo alichopewa kujikwamua kimaisha na kumsaidia sana hatimaye kuondoa kudharaulika kwa jamii.
Hata hivyo, Mhe. Kanga, amesema kwamba Halmashauri imeamua kumpatia mkopo huo unatokana na asilimia 2% za watu wenye ulemavu.
Mwisho, Mhe. Kanga, ameshukuru Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Morogoro pamoja na ngazi ya Kata kwa usimamizi wa Ilani, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mhe. Abdulaaziz Abood, Uongozi wa Manispaa ya Morogoro chini ya Mstahiki Meya na Baraza la Madiwani pamoja na Uongozi wa Kata hususani Afisa Maendeleo kwa jinsi anavyofanya kazi ya kuwatambua watu wenye ulemavu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kigurunyembe, Ndug Mchimba , amesema kutokana na kumfahamu kijana huyo,anaamini kwamba mama kijana huyo atafanya biashara ya usafiri wa bajaji na atapata kipato na ataweza kurejesha mkopo huo kwa wakati ili watu wengine pia waweze kukopa na kunufaika.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Bajaji, Sanga, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, namna inavyowajali na kuweza kuwapatia mikopo kutokana na jamii kutowatambua na kwamba wao ni wakusaidiwa na kubebwa mara kwa mara tu na hawawezi kufanya lolote.
Sanga, amesema Serikali imewatambua na kuwathamini watu wenye ulemavu na kuahidi kwamba chombo hicho ataenda kukitumia kikamilifu katika kuzalisha mali na kujikwamua kimaisha na kiuchumi na kujikomboa katika maendeleo na kuwa katika hali nzuri.
Post a Comment