Header Ads

DC MSANDO AAGIZA MANISPAA YA MOROGORO KUWEKA MIKAKATI DHABITI YA UKUSANYAJI MAPATO.


MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, ameitaka Manispaa ya Morogoro kuweka mikakati dhabiti ya ukusanyaji wa mapato ikiwamo kutumia vyanzo vipya badala ya kuangalia vyanzo ambavyo vimezoeleka.

“Ninawaomba sana kusimamia na kuongeza nguvu katika kusimamia  ukusanyaji wa mapato, tukipata mapato mazuri maana yake tunaenda kutatua kero za maendeleo ikiwemo Miundombinu, afya na elimu nk, tusikariri vyanzo, tunatakiwa kuwa na vyanzo vipya ambavyo tunadhani haviwezi kutusaidia lakini tukiviwekea mikakati mizuri tutakusanya na mapato yetu yataongezeka ”. Amesema DC Msando.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya wadau wa maendeleo, DC Msando, amesema kuwa Manispaa ikikusanya fedha nyingi basi miradi ya maendeleo itafanyika na fedha nyengine zitatumika katika kutatua kero za wananchi.

Pamoja na hayo, DC Msando, amewataka watendaji kuongeza uwezo wa kukusanya mapato kwa kuwa mstari wa mbele wa kutambua vyanzo vya mapato vilivyo katika maeneo yao.

“Tujikite katika kukusanya mapato, hii ndio njia nzuri itakayotusaidia sisi kuwahudumia wananchi kwa urahisi, tukitumia  mapato ya ndani tunaweza kutatua kero za  wananchi wetu na wananchi watafurahi lakini pia tutapata baraka za Mwenyezi Mungu”. Ameongeza DC Msando.

Mbali na mapato, DC Msando, ameyataka Mabaraza ya ardhi ya Kata yawezeshwe ili yaweze kusimamia kazi zao ipasavyo ikiwamo kutoa haki stahiki kwa wananchi wao.

Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga,amesema watahakikisha wanaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili viweze kusimamia miradi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Jeremiah Lubeleje, amesema wamepokea maelekezo na tayari washachukua hatua madhubuti ya kuhakikisha mapato yanaongezeka.

Lubeleje , amesema kuhusu chanzo cha Gymkhana, Manispaa imeshatoa maelekezo kwamba mto yeyote atakaye mpata mwekezaji mwenye utayari basi afike nae Ofisini kwa ajili ya mazungumzo kuona jinsi watakavyoweza kufanya nae kazi.

Kuhusu Machinga, Lubeleje, amesema Manispaa imetenga milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya machinga ambapo hadi sasa jumla ya vibanda 88 vimeshaanza kujengwa Mtaa Mfupi maeneo ya faya.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.