Header Ads

WAKODISHA MAGARI (TOURS) MASIKA RUKSA STENDI YA ZAMANI, DC MSANDO, MKURUGENZI WA MANISPAA WATOA MAELEKEZO.

 








MKUU wa Wilaya ya  Morogoro, Mhe. Albert Msando, kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, wametoa maelekezo kwa umoja wa wakodisha magari  waliopo eneo la Masika juu ya kuhamia eneo la Stendi ya zamani ya daladala Mjini kati.

Kauli hizo wamezitoa leo Januari 31/2022 wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya akiambatana na Kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Morogoro  ya kukagua maeneo ya biashara yanayojengwa vibanda, miundombinu pamoja na maeneo ambayo watumiaji wa biashara wamekuwa wakiyatumia ambayo yapo katika hifadhi ya barabara na kuongeza vibanda.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe.Albert Msando, amesema kuwa muda na wakati wowote watahamia katika stendi ya zamani ili kupisha eneo hilo kwa matumizi mengine.

DC Msando, amesema kuwa, wanataka kuona Mji unapangika hivyo wanatakiwa kuhama eneo walilopo sasa na kwenda Mjini lakini kwa utaratibu maalum watakaopewa.

"Hapa tunawahamisha, tunataka mfanye kazi eneo zuri na mjitangaze, mkiwa katika mtawanyiko ngumu kupata wateja, lakini hata kama kuna watu wengine ambao sio wahudumu katika biashara hizi watawaharibia soko maana hata wakisababisha ajali uaminifu kwenu utapungua, mkikaa eneo moja tutawajua wateja na wale waharifu tutawabaini moja kwa moja, maelekezo tutawapa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kabla ya Uongozi wa LATRA hawajawapangia eneo hilo" Amesem  DC Msando.

Aidha, DC Msando, amesema utaratibu wa kufanya kazi eneo la stendi ya zamani watatakiwa kuijiorodhesha na majina yao na magari yao na namba zao zikapitia kwa Mkurugenzi kisha baada ya hapo LATRA watasimamia.

"Hapa naomba lieleweke, sitotaka kusikia mmevuruga utaratibu, fanyeni kazi mliyoiomba, Mkurugenzi wa Manispaa ndiye atakayepitisha majina yenu, sitaki kusikia LATRA wamewapangia eneo bila Mkurugenzi kuhisishwa LATRA na Manispaa muwe kitu kimoja kufanikisha mpango huu" Ameongeza DC Msando.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema kuwa eneo wanalopangiwa wasigeuze kuwa stendi ya kupanda na kushuka,bali wapange magari yao kwa utaratibu na yaonekane kama ni magari yanayokodishwa.

"Tunawaruhusu lakini msigeuze stendi, isije leo na keshokutwa tukaonekana tumewatoa watu fulani harafu nyie mnafanya, tunataka matumizi yenu yawe tofauti,msilundike  magari, wekeni magari kwa mpangilio mzuri kama mnavyopanga hapa masika, taratibu nyengine  zote tutashirikishana ili tuanze zoezi letu mara moja " Amesema Machele.

Katika hatua nyengine, Mwenyekiti wa mpito wa magari hayo ya usafiri wa kukodi, Johnson Manga, amempongeza Mkuu wa Wilaya na Mkuugenzi kwa kuwapa kipaumbele cha kufanya biashara zao katika eneo rafiki huku akiahidi kutokwenda kinyume na maombi yao.

 

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.