Header Ads

DC MSANDO AHIMIZA UPANDAJI WA MITI UPEWE KIPAUMBELE.


MKUU  wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, ameitaka Manispaa ya Morogoro kujielekeza katika  upandaji wa Miti ili kulinda mazingira ikiwa ni mkakati wa Kitaifa ya  kuifanya nchi kuwa ya Kijani.

Hayo ameyazungumza  Januari 27/2022 katika Kikao Maalum (Bajeti) cha Kamati ya ushauri wa Wilaya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika Ukumbi wa Mikutano wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu.

DC Msando, amesema  kuwa anatamani kuona Wilaya ya Morogoro inakuwa ya kijani ,hivyo ameitaka Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na wananchi wao kuona kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake kupanda miti katika eneo lake na kuitunza hali ambayo itasaidia kupambana na na mabadiliko ya Tabia Nchi na upatikanaji wa maji katika vyanzo vya maji.

"Ili tufanikishe hili, kipaumbele cha kwanza kiwe mazingira, mazingira yakiwa hatarishi hata hii mipango mengine tunayotaka kuifanya haitafanikiwa" Ameongeza DC Msando.

Aidha, ameitaka Manispaa ya Morogoro kuhakikisha inatenga bajeti ya kutosha ya upandaji wa miti ili kuongeza ukijani lakini kulinda vyanzo vya maji.

Katika hatua nyengine, amitaka Manispaa ya Morogoro kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato katika kujiletea maendeleo.

Pia, ameiomba Jamii kufanya kazi za uzalishaji kwa jithada na kulipa kodi pamoja na kutumia  vizuri fursa zinazotolewa na serikali makini inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, katika kuona Morogoro inakuwa kwa kasi, amesema wataendelea kupokea ushauri mbalimbali kutoka kwa wadau na kuufanyia kazi ili kuweza kufikia mafanikio.

Mwisho, DC Msando, amesisitiza suala la wazazi kuwapeleka watoto shule kwani hakuna tena kikwazo kwakuwa sasa miundombinu ya shule imewekwa vizuri kufuatia Rais Mhe. Samia Suluhu Hassani, kuiingizia Manispaa ya Morogoro Bilioni 1 na Milioni 720 pesa ambazo zimekamilisha ujenzi wa vyumba vipya  vya madarasa 86.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.