MANISPAA YA MOROGORO YAENDESHA ZOEZI LA UKUSANYAJI TAARIFA ZA ANWANI ZA MAKAZI KWA KATA 8.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro, imeendesha zoezi la ukusanyaji wa Taarifa za anwani za makazi katika Kata 8 kati ya Kata 29 zilizopo katika Manispaa hiyo.
Akizungumza
katika mafunzo ya kujenga
uelewa kwa viongozi, watendaji na wataalam wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa
anwani za makazi na postikodi, Mratibu wa zoezi hilo Manispaa ya Morogoro ,
Jackline Mushi, amesema zoezi hilo lilianza tarehe Desemba 19/2021 hadi Desemba
23/2021.
Mushi, amesema kuwa zoezi hilo lilifanikiwa kwa ushirikiano mzuri
walioupata kutoka Ofisi za Kata , Mitaa na Wenyeviti wa Mitaa husika.
Aidha, amesema katika zoezi hilo jumla ya Anwani 4437 zilikusanywa
katika Kata 8 ambazo zoezi hilo lilifanyika.
“Tumefanya zoezi hili kwa ushirikiano mkubwa wa Ofisi za Kata husika, kwakweli tumefanikiwa kwa asilimia kubwa , huduma zote zinazopatikana katika kata hizi 8, zipo katika Mfumo wa Anwani za makazi (NAPA), lakini tutahakikisha tunafikia kata zote 21 zilizobakia ” Amesema Mushi.
Kata ambazo zimefanya zoezi hilo ni pamoja na Kata ya Boma, Mji
Mkuu, Mlimani, Mbuyuni, Sultan Area, Kingo, Mji Mpya , na Kata ya Sabasaba.
Amesema kuwa matarajio yao ni kubandika namba katika nyumba
zilizowekwa Anwani za makazi katika Kata 8 ambapo namba zipo na mchakato wa kuzibandika
unaendelea, kuhamasisha wadau mbalimbali katika kuchangia zoezi la uwekaji
Anwani za makazi, kuendelea na zoezi uwekaji wa Anwani za makazi katika Kata 21
zilizobakia pamoja na Halmsahauri kuipa kipaumbele katika kutemnga vifungu
katika bajeti za kila mwaka za utekelezaji wa Anwani za makazi.
Mwisho, ametoa shukrani za dhati na za kipekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufanikisha uwekaji wa Anwani za Makazi na kuiomba Wizara ya Habari kuendelea kutoa ufadhili ili kufanikisha zoezi hilo.
Post a Comment