Header Ads

MHE. MZERU KUKABIDHI MIFUKO 100 YA SARUJI SHULE YA SEKONDARI LUPANGA MANISPAA YA MOROGORO KWA AJILI YA UKARABATI WA MADARASA .


Diwani wa Kata ya Kilakala , Mhe. Marco Kanga (kushoto ) akiwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Norah Mzeru (kulia) katika madarasa mapya ya UVIKO-19 Shule ya Sekondari upanga.

Madarasa mapya ya UVIKO-19 Shule ya Sekondari Lupanga.

Wanafunzi wakiwa wameshawasili madarasa mapya ya UVIKO-19 Shule ya Sekondari Lupanga Kata ya Kilakala.

Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza Shule ya Sekondari Lupanga.

Mhe. Mzeru, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari , Lupanga.

Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga, akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Lupanga.

Mhe. Mzeru akiwa na Uongozi wa Shule ya Sekondari Mzumbe pamoja na wanafunzi .

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, Mhe. Norah Mzeru, anatarajia kukabidhi Mifuko 100 ya Saruji Shule ya Sekondari Lupanga iliyopo Kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ambayo yameonekana kuchakaa ili yaendane na madarasa mapya.

Kauli hiyo ameitoa leo Januari 17/2022 katika ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea madarasa mapya yaliyojengwa  na fedha za   Maendeleo  na ustawi wa Taifa na Mapambano  dhidi ya UVIKO-19 pamoja na kufanya ziara Shule ya Sekondari Mzumbe iliyoshika nafasi ya 10 Kitaifa katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Mzeru, amesema kuwa ameamua kutoa Fedha zake binafsi kununua mifuko hiyo lengo likiwa ni kusaidia kufanikisha ukarabati wa madarasa ambayo yameonekana kuchakaa ili yaendane na madarasa mapya na wanafunzi wasome katika mazingira rafiki yenye kuvutia.

Mhe. Mzeru,  amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidiii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na kwamba atakuwa mstari wa mbele kuwasaidia katika kutatua changamoto zinazo wakabili kwa kadri atakavyoweza kujaliwa.

Katika hatua nyengine, Mhe. Mzeru, amewataka Wakuu wa Shule na Kamati za shule Mkoa wa Morogoro  kuzingatia Miongozo ya Serikali katika kuwachangisha fedha wazazi wa wanafunzi wanaonza kidato cha kwanza na sio kuchanga fedha ambazo hazina kibali cha michango kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

" Nipo hapa kukagua shule ya Lupanga , nimeridhishwa na ujenzi wa madarasa haya , nimpongeze Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kweli fedha zimetumika vizuri na sina mashaka kabisa naamini sasa ufaulu utaongezeka kutoka nafasi ya 5 Kimanispaa na kuingia 3 bora au ya kwanza kabisa katika matokeo yajayo" Amesema Mhe. Mzeru.

Naye Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga, amemshukuru Mhe. Mzeru na huku akisema kuwa  kitendo cha Mhe. mzeru kutoa mifuko hiyo ya saruji kinaonesha ni jinsi gani Mhe. Mzeru  anaunga mkono Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassani ya kujenga  miundo mbinu bora ya elimu na kuwezesha wanafunzi kusoma bila shida.

Hata hivyo,  Mkuu wa Shule ya Lupanga, Flora Ndunguru, amesema kuwa Msaada huo utasaidia kutatua changamoto waliyo nayo ya uchakavu wa madarasa .

Amesema wanatarajia kupokea wanafunzi 274 lakini mpaka sasa ni wanafunzi 100 wameshawasili lakini mpaka wiki inamalizika anaamini wanafunzi wote watakuwa wamewasili shuleni hapo kuanza masomo yao.

Kwa upande wa  mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliye jitambulisha kwa jina la Theresia Minja, ametoa pongezei kwa Rais Samia na kumshukuru Mbunge Mzeru , kwa moyo alio onyesha kujitoa kuwasaidia kutatua changamoto hiyo na kumuahidi kuwa watasoma kwa bidii na
Kufaulu kwa asilimia 100 katika mitihani yao pamoja na kuongeza ufaulu shuleni hapo.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.