Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAKIKABIDHI KIKUNDI CHA BOMSATE MSAVU BODABODA 10 ZENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 25,800,000/=.

MANISPAA ya  Morogoro, imekabidhi  Bodaboda 10 zenye thamani ya shilingi Milioni 25,800,000/= kwa Kikundi cha BOMSATE kilichopo Kata ya Mafisa Mtaa wa White House chenye Maskani yake eneo la Stendi ya Mabasi Msavu kwa lengo la kuwawezesha katika kujikwamua kiuchumi.

Tukio hilo la kukabidhi Bodaboda limefanyika Desemba 30/2021 katika eneo la Yard Magereza likishuhudiwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa White House, Ndg. Said Yassin, pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mafisa, Jesca Matandura.

Akikabidhi Bodaboda hizo, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii, Rutahiwa John, amesema kuwa uwezeshwaji huo unatokana na fedha za makusanyo ya ndani ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kutenga asilimia 10 ya bajeti ya Halamshauri kila mwaka kwa ajili ya kuviwezesha vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.

"Rais wetu Samia Suluhu Hassan alielekeza fedha hizi ambazo wanapewa makundi haya , zitolewe bila riba ili kila mmoja awe  mnufaika, nitumie fursa hii kumpongeza Mkurugenzi wetu Ally Machela, Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kusimamia maelekezo haya vizuri na leo hii tunaona Vijana wetu wakinufaika na mpango huu, raia yangu wanapopata mkopo huu warejeshe fedha kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika" Amesema Rutahiwa.

Rutahiwa, amesema kuwa katika bodaboda hizo walizopatiwa Vijana hao inakamilisha jumla ya Bodaboda 30 ambazo mpaka sasa wameshapatiwa.

Mwisho, amesema Manispaa ya Morogoro, inaendelea kuhamasisha jamii juu ya uwepo wa asilimia 10 kwa ajili ya kuwawezesha na kuinua Wananchi kiuchumi kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM ) ya mwaka 2020.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa White House Kata ya Mafisa ambapo kikunci hicho kipo katika eneo lake la utawala, ameupongeza Uongozi wa Manispaa ya Morogoro ukiongozwa na Meya, Madiwani , Mkurugenzi,pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo na watumishi kwa kuona umuhimu wa kusaidia jamii katika kuwainua kiuchumi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa BOMSATE, Awadhi Hamis, amesema mkopo walioupata watahakikisha wanautumia vizuri na kufanya marejesho kwa wakati.




No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.