Header Ads

Manispaa ya Morogoro mbioni kukamilisha Ujenzi wa Choo cha Mtoto wa Kike.


Choo cha Mtoto wa Kike kinachoendelea na Ujenzi kilichopo Shule ya Sekondari Tubuyu.

Upande huu wa Choo ni kwa ajili ya Wanafunzi wakike wenye ulemavu.
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, (katikati) akimpa maelekezo Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma Gwisu, (kulia) Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro, Dkt Janeth Barongo.
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba akikagua ujenzi wa Chemba ya Choo hicho unaoendelea.
Ujenzi wa Chemba ya Choo ukiendelea.


HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro katika mapato yake ya ndani ipo mbioni kukamilisha Choo cha Mtoto wa kike chenye thamani ya Shilingi Milioni 35 kilichopo Shule ya SekondariTubuyu, ikiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kike kuweza kukamilisha haja zao kipindi cha hedhi.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 15, 2020, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, Mara baada ya kukagua mradi huo wa ujenzi huo, amesema kwa kuwa Wanawake wengi wamekuwa na changamoto nyingi katika mabadiliko ya kimwili wameona sasa ipo  haja ya Shule zilizopo Manispaa ya Morogoro kujenga Vyoo vya Mtoto wa kike mara baada ya kilichopo kukamilika.

“Wanafunzi wengi wa kike  wanachangamoto hususani katika kipindi cha siku zao za  hedhi, wanapoingia katika siku zao, hivyo wengi wanashindwa kufika shule wanapoingia katika hedhi kwa hali waliyonayo, hivyo katika fedha nilizotenga kwa ajili ya elimu Sokondari , tumeona ni vyema tukawajengea Vyoo hivi viwasaidie katika kujikinga na kujisafisha kipindi wanapoingia katika hedhi, niwaombe Wanafunzi wote wasiwe watoro shuleni watambue hedhi sio ugonjwa bali ni mabadiliko ya mfumo wa uzazi, vyoo hivi vitakuwa na bafu maalumu litakalo kuwa na  sehemu maalumu ya kutunzia vifaa vyote muhimu , ikiwemo taulo za Mtoto wa kike pamoja na kio cha kujiangalia na sabuni kwa ajili ya kunawia na kuogea”Amesema Sheilla.

Amesema kuwa tafiti iti zinaonesha kuwa mtoto wa kike anakosa masomo siku 4 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa huduma ya vyoo bora na maji salama na safi shuleni ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Miongoni mwa malengo hayo ni lile lengo namba 4: linalohamasisha kuhusu Elimu Bora, Lengo la 5: linalo hamasisha juu ya Usawa wa Kijinsi na lengo namba 6: kuhusu Maji Safi na Salama.

“Huu ni mwanzo tu, tunataka choo hiki kiwe cha mfano katika Mkoa wetu wa Morogoro, ni matumani yangu baada ya kukamilika kwa choo hiki tutaendelea na ujenzi wa vyoo vyengine ili kuhakikisha mtoto wa kike anawekewa mzingira rafiki anapokuwa shuleni ili aweze kuhudhuria masomo yake kwa ukamilifu kama ilivyokuwa kwa mtoto wa kiume kwani “Ukimkomboa mtoto wa kike umekomboa Taifa zima” Ameongeza Sheilla.

Amesema kuwa ujenzi wa Vyoo vya Mtoto wa kike imetokana na changamoto zinazoendelea kuwakabili wanafunzi kukosa vyoo bora na maji salama na safi shuleni. Tatizo hili linawaathiri watoto wa kike zaidi  kwani wanashindwa kujistiri hasa wanapokuwa katika siku zao za hedhi katika mazingira ya shuleni.

Naye Afisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Morogoro, Dkt. Janeth Barongo, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa mbinu nzuri ya kuwasaidia wanafunzi wa Kike shuleni.
Amesema Vyoo hivyo vitapunguza utoro kwa watoto wa kike kwani wengi wamekuwa wakishindwa kufika shule wakati wa hedhi lakini baada ya ujenzi huo utasaidia sana na wanafunzi watahuduhuria shule wakiwa katika hali hiyo maana ipo sehemu salama kwao katika kujisafisha na kujilinda.

Ameowaomba Wazazi kuwahimiza watoto kwenda shule mara baada ya kupata hedhi kwani mabadiliko hayo yanazuilika wakiwa shuleni.

“Mkurugenzi wetu amekuja na mbinu nzuri sana, kwakweli hiki choo kitakuwa cha mfano katika Mkoa wetu wa Morogoro, ambapo kitaiadia kupunguza utoro kwa watoto wa kike wanaoingia katika siku zao (hedhi), kumekuwa na changamoto wanafunzi kubeba pedi kwenye begin a kwenda nazo shule wengine wanaenda kuomba ofisini , lakini kwa hali hii ni vigumu hata kutambua mtu yupo katika hali gani maana vifaa vyote vitakuwa chooni ni yeye kwenda na kujihudumia”Amesema Dkt. Barongo.

Choo hicho kina jumla ya matundu 12.







No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.