DC CHONJO ASHUSHA MAELEKZO NA KUWATAKA WAMILIKI WA HOTELI KUWA WAKALI KATIKA KUWAPOKEA RAIA WA KIGENI.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, akifungua mkutano huo katika kumkaribisha Mkuu wa Wilaya. |
Mmoja wa Wamiliki wa Hoteli akichangia hoja katika Mkutano huo. |
Samson Nyakinga, Mkaguzi wa Uhamiaji Wilaya ya Morogoro na Kaimu Afisa Uhamiaji akitoa maelekezo juu ya kushirikiana kuwabaini raia wa kigeni katika maeneo ya Hoteli na nyumba za wageni. |
Wamiliki na Mameneja wa Hoteli wakifuatilia kwa umakini Mkutano wa Mkuu wa Wialaya wa maagizo juu ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA. |
MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amekutana na
Wamiliki pamoja na Meneja wa Hoteli Wilayani Morogoro kwa ajili ya kuwapatia
elimu pamoja na maelekezo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Magufuli, juu ya kuwapokea raia wa kigeni katika Hoteli zao ikiwa
na lengo la kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Mkutano huo umefanyika leo Aprili 3, 2020 katika Ukumbi wa
Mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Wamiliki hao na Mameneja wa Hoteli , amesema lengo
la mkutano huo ni kuwapa maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli juu ya kuwapokea raia wa kigeni katika
Hoteli zao ikiwa na lengo la kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Amesema kumekuwa na utaratibu wa kuwakumbatia watu wasio
julikana katika nyumba za kulala Wageni hususani katika Hoteli jambo ambalo ni
baya sana hasa katika kipindi hiki cha kupambana na vita dhidi ya Ugonjwa wa
CORONA.
Chonjo, amesema ni wakati wa kushirikiana na kuwa kitu
kimoja kati ya Serikali na Wamiliki wa Hoteli kwa ajili ya kuwachunga na kuwatolea
maelezo raia na washukiwa wanaoingia katika Hoteli zao kwa kuwawekea ulinzi
endapo watawabaini ili kutoeneza ugonjwa huo.
“Tumeitana hapa kwa lengo moja, Mhe. Rais Dkt John Magufuli
ameshatoa maelekezo kwa Hoteli zote jinsi ya kuweka umakini na wageni wanaotoka
nchi zilizo na historia ya Ugonjwa huo, kwahiyo tunatakiwa tushirikiane kwa
pamoja na tutoe ushirikiano wa kuweka mazingira kwa washukiwa hao, kama utaona
mtu haeleweki toa taarifa au ameingia katika Hoteli yako ni raia wa kigeni
muhifadhi katika chumba chenye huduma zote ndani kwa muda wa siku 14 na asitoke nje baada ya
hapo piga simu kwa wataalamu wa afya watakuja kumuangalia kitaalamu na baada ya
siku 14 kama zitaonekana dalili za Ugonjwa huo atachukuliwa na Wataalamu
kufikishwa katika Karantini zetu tulizozitenga maeneo, hawa sio kwamba wana
ugonjwa ila tahadhari ni muhimu na chumba chake hakikisheni muhudumu haingii
ndani , wala ndugu pamoja na familia zao na huduma za chakula anatakiwa awekewe nje ya mlango na kumgongea ili kukifuata na upande wa nguo zao lazima zifuliwe kwa dawa na kuwekwa katika vikapu
zikikauka zipelekwe mlangoni kama ilivyo huduma nyengine , lakini baada ya mtu huyo kumaliza karantini
hapo Hotelini chumba chake kitatakiwa kufanyiwa Farmigation ya hali ya juu na
huyo mtu atajaza fomu ya kuonyesha kwamba alikuwa Karantini na yupo tayari
kuwepo uraiani” Amesema DC Chonjo.
Aidha, amewatahadharisha Wamiliki kuacha tama ya pesa badala
yake wawe makini katika kutanguliza afya za wahudumu wao pamoja na za Wananchi
kwa ujumla kwani wanaweza kuwa na tamaa ya kupokea fedha nyingi wakati huo
wanaleta ugonjwa na kuhatarisha maisha ya watu wengine.
Pia amesema ni vyema kujenga ushirikiano mzuri baina ya
Wamiliki wa Hoteli, Maafisa Uhamiaji pamoja na Wataalamu wa afya ili wanapombaini
mtu haeleweki au ana dalili za ugonjwa huo wakatoa taarifa mapema sana ili
hatua za kitaalamu ziweze kuchukuliwa.
Hata hivyo,amewataka
Wamiliki wa Hoteli wote kuanzia tarehe 6, Aprili siku ya Jumatatu , kila mmiliki awe ametoa
taarifa ya huduma za bei katika vyumba vya kulala kwa Hoteli nzima na kukabidhi
timu ya Wataalamu watakao pita mitaani kukusanya taarifa hizo ili wale
wanaotaka kwenda kupata huduma kama itatokea anawekwa mtu Karantini basi alipe
kulingana na uwezo wake wa fedha katika upatikanaji wa huduma hizo ili isije
kuleta shida kwa wamilki wa Hoteli baada ya kushindwa kulipa huduma .
Amesema kuwa baada ya ugoinjwa huo kuingia hapa nchini, Wilaya ya Morogoro iliunda Kamati za Karantini, hivyo ni jukumu sasa la Kamati hiyo kuanza
kufuatilia bei za vyumba vyote kwa kila
Hoteli ili kuweza kuona jinsi ya
kuwasaidia Wageni wanaotaka Hoteli kwa
bei tofauti tofauti kulingana na uwezo wake wa kifedha.
Katika kuhitimisha mkutano huo, amesema kama watu wote watamuomba
Mwenyezi Mungu na kuzingatia maelekezo
ya Wataalamu pamoja na Viongozi wa Ngazi za juu na kufuata maelekezo yote basi ugonjwa huo kwa Wilaya ya Morogoro hautafika .
Katika hatua nyengine, DC Chonjo, aliwataka Waganga wakuu wa
Manispaa ya Morogoro pamoja na Morogoro Vijini kuwasilisha taarifa ya jinsi
walivyochukua hatua za kupambana na Ugonjwa wa CORONA.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Morogoro Vijijini, Dr. Robert
Manyenyere , amesema wao walitumia njia za kutoa elimu katika maeneo yote yenye
mikusanyiko ya watu , kutenga eneo la Karantini katika Kituo cha afya cha Ngerengere,
kutenga eneo la Karantini katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, pamoja na kuweka
kituo cha Karantini katika Mradi wa Mwendokasi kwani eneo hilo limekuwa na
wageni wanaoendelea na ujenzi huo.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Gosbert
Kalunde, amesema Manispaa ya Morogoro imetoa elimu katika meneo yote yenye
mkusanyiko ikiwamo Nyumba za wageni, mama ntilie ,Matangazo katika Vyombo vya Habari, vituo vya Bajaji, Bodaboda,
Madukani, Stendi za Daladala pamoja na Stendi kubwa ya Mabasi yaendayo Mikoani ya Msamvu lengo likiwa kuwaelimisha
wananchi jinsi ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Amesema tayari Manispaa ilishaanda timu ya Wataalamu wa Karantini na eneo ilishatenga
lililopo katika Ujenzi wa Hospitali ya Manispaa iliyopo Kata ya Mkundi ambapo
washukiwa wote wa Ugoinjwa wa CORONA wanapekwa huko kwa jili ya vipimo vya
awali.
Pia amesema wamenunua vifaa tiba kwa kuwakabidhi wauguzi waliopo katika Vituo vya afya pamoja na wale waliopo katika Karantini hiyo kuvitumia endapo watapata mshukiwa wa ugonjwa huo.
Licha ya jitihada hizo, lakini amesema wapo viongozi wa
Manispaa kwa fedha zao wenyewe waliamua kuiunga Mkono Serikali kwa kugawa ndoo
za maji , sabuni pamoja na vitakasa mikono kwa jili ya kuwakinga wananchi wao na
ugonjwa huo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla
Lukuba, amesema baada ya agizo la Waziri Mkuu, Mh Kassim Majaliwa la kuwataka wafanyabiashara kuuza
vifaa tiba kwa bei elekezi, yeye pamoja na timu yake ya Wataalamu walitembelea
maduka hayo na kupiga faini baadhi ya maduka kwa kukiuka agizo la Waziri na
kutoza faini kwa upande wa magari ambayo yalikiuka pia maagizo ya kuwawekea maji
sabuni na vitakasa mikono abaria wao.
Paul Haule ambaye ni Mmiliki wa Bambo Guest House,
amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa
maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kumpa ushirikiano katika mapambano dhidi
ya Ugonjwa wa CORONA.
“Tunampongeza Mkuu wa Wilaya hakika kikao hiki ni chakujenga
kwa pamoja, ugonjwa huu unaua ndugu zetu wanateketea katika Mataifa mengine , kwahiyo tukuhakikishie Mkuu wetu wa Wilaya maagizo kwa pamoja tumeyapokea na tunakwenda kuyafanyia kazi , wote
tukishirikiana kwa pamoja ugonjwa huu utakuwa ni historia kwetu wananchi wa
Morogoro” Amesema Haule.
Post a Comment