Mkurugenzi Manispaa Morogoro achukua uamuzi mzito juu ya Wazururaji Stendi za Mabasi na Masoko.
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Sheilla Lukuba akiteta jambo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dr.Dr. Kusirye Ukio katika Stendi ya Mabasi Msamvu wakati wa ziara ya kukagua zoezi la uwekaji ndoo katika Mabasi na upuliziaji wa dawa pamoja na Vitakasa mikono. Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Sheilla Lukuba, akinawa mikono wakati wa kuingia katika Kituo cha Mabasi Msavu wakati wa ziara ya kukagua ndoo za kunawia maji pamoja na vitakasa mikono . Kaimu Afisa Afya Mkoa wa Morogoro, Prisca Gallet (kulia) akizungumza jambo na Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Sheilla Lukuba, (katikati) Meneja wa Stendi ya Mabasi Msavu, Gilbert Changarima. Zoezi la upuliziaji dawa katika magari likiendelea katika Kituo cha Mabasi Msamvu. |
MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amepiga marufuku watu kuzurura hovyo katika Kituo cha Mabasi Msavu pamoja na Masoko ikiwa ni moja ya kupunguza mikusanyiko ya watu katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa CORONA.
Hayo, ameyazungumza leo, Aprili 8, 2020, mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Mabasi Stendi ya Msavu pamoja na Soko la Mawenzi.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema kumekuwa na wimbi la wazururaji katika Stendi ya Mabasi Msavu pamoja na Masoko bila kuwa na shughuli maalumu ya kufanya na kusababisha msongamano wa watu wanaopata huduma.
Amesema kuanzia leo Aprili 8,2020 ni marufuku mtu kuingia Stendi ya Msavu na Masoko bila kuwa na kazi ya kufanya na watakao kaidi watachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kukamatwa na kufikishwa Mahakamani.
“Nimekuja hapa Stendi ya Msavu, kwa kweli bado sijaridhishwa na utaratibu uliopo, kuna watu wengi sana humu lakini ukija kuangalia wengi hawana shughuli za kufanya hivyo ni vigumu kutambua wapi wabaya na wapi wazuri, tushazungumza na Mawakala wa Mabasi hapa Msamvu na tumekubaliana kwamba kuanzia leo wanaotakiwa kuingia humu ni wale wenye vitambulisho, Sare na wenye kazi maalumu ikiwemo Wajasiriamali wadogo wadogo wenye Vitambulisho na wale wanaotambulika , tufuatae agizo hili bila shuruti ikishindikana kujiongoza tutawaongoza kwa kutumia nguvu, tuanataka Stendi zetu na Masoko yetu tusiwe na misongamano isiyo na msingi wakati mwengine tunakaribisha wezi wenyewe bila kujijua , tuna janga la CORONA tuzingatie pia miongozo ya Wataalamu wa afya pamoja na Viongozi wetu wa ngazi za juu wanaotoa maagizo”Amesema Sheilla.
Aidha, amesema wapo katika hatua za kuweka Kituo kidogo cha kutolea huduma za afya katika Stendi ya Mabasi Msavu ili kutoa huduma kwa wale wanojisikia vibaya na washukiwa wa ugonjwa wa CORONA.
“Nimemuagiza Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, kuweka kituo cha afya hapa Msavu, jana nilipigiwa simu kuwa kuna Basi kubwa limeelekea Hospitali ya Mkoa tena kwa King’ora cha polisi likimpeleka mtu baada ya kushukiwa na ugonjwa wa Corona, kwa kweli jambo kama lile sio jema kabisa na linaweza kuleta taharuki kwa Wananchi pamoja na kupoteza muda kwa wasafiri wengine, hivyo tumeona ni vyema tukawa na kituo cha afya kidogo hapa Msavu kwa ajili ya kusaidia matukio kama haya yanayojitokeza , kikubwa madereva na makondakta tuliwapatia elimu na kuwaelekeza nini cha kufanya kama watapata mshukiwa wa Ugonjwa wa CORONA , kuna namba tumezitoa ambazo ni 0754386037,0714199919 AU 0622181494 kwa msaada wa kiafya, hivyo wanapoona kuna mtu mwenye dalili au hata mtaani watupigie hizo namba wataalamu wa afya watafanya kazi zao”Ameongeza Sheilla.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dr Kusirye Ukio, amesema kwa sasa elimu inazidi kutolewa lakini ni vyema nguvu kubwa sasa ikaelekezwa katika utoaji wa elimu juu ya mikusanyiko ya watu kwani bado kuna hitajika elimu kwa upande huo.
“Tumekuwa tukishirikiana vyema na Wataalamu wa Manispaa ya Morogoro, ndio maana leo tupo hapa na Mkurugenzi tukishauriana baadhi ya mambo katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virus vya CORONA, tumeshatoa elimu sana, kikubwa sasa nguvu zetu tunaelekeza kwenye mikusanyiko ya watu hususani katika Vituo vya Mabasi pamoja na Masoko ambapo kumekuwa na watu wengi sana” Amesema Dr. Ukio.
Pia mesema wanaanda utaratibu kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, wa kugawa fomu za uchunguzi kwa kila basi linaloingia Stendi ya Msavu na ili kukaguliwa kama limepulizwa dawa na kupewa fomu zitakazojazwa zikiwa chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya kwa kushirikiana na Askari Polisi wa Msamvu .
Katika hatua nyengine, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, alivamia Soko la Mawenzi na kutoa agizo kama alilolitoa Stendi ya Msavu na kumuagiza Mkuu wa Masoko kusimamia agizo la kamata kamata la wazururaji wote Masokoni kuanzia leo Aprili 8,2020.
Amesema hali ya Soko hairidhishi , hivyo amemuagiza Mkuu wa Massoko wa Manispaa ya Morogoro kuongeza nguvu ya usafi pamoja na kumuandikia mahitaji ya vifaa vinavyotakiwa katika Masoko kwa ajili ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
“”Soko hili bado sijaridhishwa nalo, wenzenu kule Soko la Mji Mpya ni wasafi sana , nakuomba msimamizi wa masoko shirikianeni vizuri na maafisa afya wenu wa Soko pamoja na wa Manispaa kuhakikisha kila baada ya vibanda 3 kuwe na ndoo ya kunawia maji na sabuni, ndoo hizi hazitoshi nendeni mkatuandikie mahitaji yenu mtuletee tuwasaidie, hapa ni sokoni lakini bado vyakula vinauzwa chini ni hatari kwa walaji, tunataka usafi kwanza, tukiwa wasafi hata ugonjwa huu wa CORONA itakuwa vigumu kutufikia lakini hakikisheni mnakwenda kuwadhibiti wazururaji maana kuna watu wengine hawana shughuli za kufanya huku Sokoni lakini wapo mnawalea, tufike mahala tusema inatosha mikusanyiko imepigwa marufuku tutekeleze agizo la Wataalamu wa afya na Viongozi wetu wanayotuambia, tusitumie nguvu katika afya zetu mkishindwa kujiongoza naleta Jeshi langu la akiba hapa tuanze kukimbizana,nawapa siku moja leo muwe mmeweka utaratibu mzuri hapa sokoni nikirudi tena ni vitendo tuu” Amesema Sheilla.
Kwa upande wa Mkuu wa Masoko, Manispaa ya Morogoro, Abdully Mkangwa, amempongeza Mkurugenzi kwa hatua alizochukua za kupiga marufu wazururaji .
“Mkurugenzi wetu amechukua uamuzi mzuri sana tunampongeza, sio kwamba sisi hatuwezi kuwakamata, hata mkituambia sasa hivi tunawakamata hawa wazururaji, lakini tunachokitaka na kukiomba kwenu mtuahakikishie hawa tunaotaka kuwakamata tukiwashika wasirudi tena , maana unaweza kuwakamata lakini kesho unawakuta mitaani jambo ambalo linatuvunja nguvu sisi, lakini kwakuwa umeshatoa agizo tutalifanyia kazi na tutaonyesha ushirikiano wa hali ya juu katika masoko yote hapa Manispaa ya Morogoro” Amesema Mkangwa.
Aidha amesema suala la kuweka ndoo kila baada ya vibanda 3 vya biashara wamelichukua na watahakikisha usafi katika soko hilo unafanyika na ndoo zinakuwa nyingi kwa ajili ya kuwakinga wananchi dhidi ya Ugonjwa wa CORONA.
Post a Comment