DC Mjema atimiza agizo la Rais JPM utoaji wa Vitambulisho kwa Wamachinga.
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Mh: Sophia Mjema, amezindua rasmi zoezi la utoaji wa Vitambulisho kwa Wamachinga kufuatia agizo la Rais JPM Jana kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Uzinduzi huo wa Vitambulisho umefanyika leo kwenye Ofisi ya Wamachinga ( KAWASO), iliyoko Mtaa wa Narung'ombe uliopo Kata ya Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi Wa habari , DC Mjema, amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha ina mnyanyua Mtanzania mnyonge hususani Wajasiriamali wadogo wadogo ikiwamo Wamachinga.
Amesema uzinduzi huo umetokana na agizo la Rais wa Tanzania, Mh: John Magufuli, la kutaka Wamachinga wote walio na mtaji chini ya Milioni 4 wapatiwe Vitambulisho.
Amewataka Wamachinga kuchangamkia fursa hiyo kwani miongoni mwa faida watakazo zipata ni pamoja na kutambulika, kuweza kukopeshwa pamoja na kufanya shughuli zao bila kubughuziwa na mtu yeyote.
" Nipende kutoa rai kwa wale watakaobainika kutoa taarifa za udanganyifu tutawachukulia hatua Kali za kisheria, Rais kasema kiwango cha mtaji chini ya Milioni 4 ,sasa tukikukuta kiwango chako kipo juu ya hicho tutalala na wewe mbele, ndio maana tunachukua taarifa kamili ili tuweze kukutambua" Amesema DC Mjema.
Amesema kuwa katika zoezi hilo wapo makini sana hivyo hawaweza kugawa Vitambulisho hivyo kama sadaka bila kukaguliwa na kutambua thamani ya mtaji pamoja na taarifa sahihi.
Pia amewataka wale wote waliopata Vitambulisho vya TRA wavitunze kwani Kamishina atawafuata kuwapa maelekezo zaidi.
Naye Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala na Diwani wa Kata ya Vingunguti, Omary Kumbilamoto, amempongeza DC Mjema huku akiahidi kulibeba suala hilo katika utoleaji wa elimu zaidi hususani katika Kata yake.
Pia amempongeza Rais John Magufuli, kwa kuonesha uthubutu wake wa kuwajali Wamachinga ambao kwa kipindi kirefu walikuwa katika changamoto za kutoa huduma zao.
" Nimpongeze Rais wetu kwa kazi nzuri kwani kutawasaidia wafanya Biashara hao kutambulika na kufanya shughuli zao katika utaratibu, pia DC Mjema nampongeza kwa kusimamia vyema agizo la Mh: Rais John Magufuli " Amesema Kumbilamoto.
Kwa upande wa mmachinga, Abdallah Kinyei, amempongeza DC Mjema kwa kazi nzuri huku akisema zoezi hilo litawasaidia wao kufanya kazi katika Mazingira tulivu.
Post a Comment