UGAWAJI WA DAWA ZA KICHOCHO NA MINYOO SHULENI KWA WANAFUNZI WENYE UMRI WA MIAKA 5 - 14 MANISPAA YA MOROGORO KUANZA KUTOLEWA.
MANISPAA ya Morogoro mbioni kugawa dawa za kinga tiba za minyoo na kichocho zoezi litakalo fanyika februari 26-27/2024 kwa shule za Msingi zikiwemo za Serikali na Binafsi.
Hayo yamesemwa februari 21/2024 na Mratibu wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele Manispaa ya Morogoro, Bi. Warialanga Nnko, kwenye mafunzo ya kutoa huduma ya dawa hizo kwa waaalimu wakuu wa shule za Msingi na waalimu wa afya yaliyofanyika Shule ya Msingi Sultan Area.
Nnko, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha zoezi hili la ugawaji wa dawa linatekelezwa vizuri ili kila mtoto/mwanafunzi aweze kupewa dawa hizo.
"Lengo la mafunzo haya ni kuwaandaa waalimu wakuu wa shule zetu za Msingi na waalimu wa afya katika kusimamia zoezi la ugawaji wa dawa za minyoo ya tumbo na kichocho kwa waafunzi wenye umri wa miaka 5-14 , lengo la utekelezaji wa mpango huu ni kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora hususani watoto wetu ambao asilimia kubwa wamekuwa wakikumbwa na magonjwa haya" Amesema Nnko.
Aidha, Nnko, amesema kuwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii maskini lakini jamii yenyewe na hata wataalam husika ama viongozi hawayapi umuhimu kulingana na madhara yake katika jamii ambapo ameyataja magonjwa hayo kama vile usubi, Matende na mabusha, Trakoma, kichocho na minyoo ya tumbo.
Naye mwezeshaji wa maada ambaye pia ni Afisa Afya Manispaa ya Morogoro, Ndimile Kilatu, amesema kichocho husababishwa na minyoo inyoitwa jamii ya Schistosoma ambao unaenezwa na konokono kwa kutoa vimelea kupitia maji yaliyotuama.
Kilatu, amesema kuwa kichocho husababisha damu kutoka kwenye njia ya mkojo na choo, na baadae inaweza kusababisha saratani ya tumbo, kibofu cha mkojo na ini.
Aidha, Kilatu, ameongeza kuwa minyoo ya tumbo imegawanyika katika aina tatu 3 nayo ni minyoo mviringo, minyoo mjeledi, na minyoo ya safura ambayo huishi kwenye udongo na husababisha mtu kuwa dhaifu na kuishiwa damu na isipotibiwa mapema inaweza kusababisha utumbo kujifunga na kifafa, pia inaweza kumfanya mtoto ashindwe kuhudhuria shule au kutoelewa vizuri.
Kwa upande wake, Dkt. Nicolous Ntabaye, amezitaja njia za kujikinga na magonjwa hayo ni pamoja na kutumia dawa za kutibu na kudhibiti magonjwa haya ambazo hutolewa kila mwaka kwa jamii iliyoathirika, kuzingatia usafi wa uso na mwili, usafi wa mazingira, kutokuoga kwenye maji yasiyo safi na yaliyotuama (bwawa), kujikinga kuumwa na inzi au mbu, na kutoa elimu ya afya ya jamii.
Naye Kaimu Afisa Elimu Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi , Said Kivufu , amesema atahakikisha anasimamia vizuri shule zote il zoezi hilo la ugawaji wa dawa lifaniiwe na kuleta mafanikio yenye tija.
Kivufu, amewataka wato huduma za dawa wazingatie mafunzo pamoja na maelekezo ya utoaji wa dawa ili yasilete madhara kwa jamii.
Miongoni mwa shule 10 zitakazopatiwa dawa za kichocho ni Shule ya Msingi Mwere A na B, Kingolwira, Mwenge, Agape, Sabasaba A na B , Kaloleni , Mwembesongo na Uhuru.
Post a Comment