KAMPENI YA CHANJO YA SURUA MANISPAA YA MOROGORO KUANZA FEBRUARI 15-18-2024
MANISPAA ya Morogoro inaratajia kutekeleza agizo la Serikali ya kampeni ya utoaji wa chanjo ya Surua Kuanzia tarehe 15 mpaka 18 ya mwezi februari 2024.
Hayo yamesemwa Februari 13/2024 na Mkuu wa Divisheni ya Afya ,Ustawi wa Jamii na Lishe Manispaa ya Morogoro, Dkt. Maneno Matawa katika ukumbi wa Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro kwenye Mafunzo ya utoaji wa chanjo hiyo kwa wataalamu wa Vituo vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Dkt. matawa, amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI imeandaa kampeni shirikishi ya kitaifa ya utoaji wa chanjo ya Surua ambayo Manispaa itaanza kutekeleza hivi karibuni ili kuweza kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa Surua kwa kuwapatia chanjo hiyo.
" Tunalo jukumu la kutoa chanjo hii mapema iwezekanavyo ili kuokoa watoto katika janga hili, niombe tusiende kufoji taarifa, tuwe na taarifa halisi za uchanjaji ili kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa huu wa Surua" Amesema Dkt. Matawa.
Mwisho amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa kipindu pindu ikiwemo kunawa kwa maji yanayotiririka, kuwa na choo bora na maji salama na kuepuka mazingira machafu yanayozunguka jamii.
Naye Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya. Dkt.Ragi Samwel, amewataka watoa chanjo kutumia mafunzo hayo kutoa huduma bora na pale wanapoona yapo maudhi madogomadogo na makubwa katika chanjo hiyo wasisite kutoa taarifa haraka ili zifanyiwe kazi.
Aidha,amesema bado kuna kasumba ya baadhi ya wananchi kukimbilia tiba mbadala badala ya kwenda vituo vya afya, huku akiwaomba sana watoa huduma kujitahidi kutoa elimu ya kutosha ili mpango huo wa utoaji wa chanjo uwe na tija,
Dkt. Ragi, amewaomba watendaji wa Kata na Mitaa kubeba jukumu la kuhakikisha zoezi hili linaenda sawa kwa kuhakikisha wanafanya uhamasishaji kwa wananchi ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo kwa wakati kutokana na ratiba ilivyo.
"Tuendelee kuwaelimisha wananchi juu ya kutoa elimu na hamasa ya kutosha kwa wananchi kuhusiana na athari za ugonjwa huo na chanjo hiyo inayotolewa na Serikali ni salama na haina malipo" Amesema Dkt. Ragi.
Naye, Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Morogoro, Philipo Bwisso, amesema kuwa magonjwa ya Surua huenezwa kwa njia ya hewa hususani pale mgonjwa anapokohoa au kupiga chafya na maambukizi huwa ni ya haraka sana hasa sehemu zenye msongamano.
"Jumla ya timu 60 zimeandaliwa timu hizo zimehusisha watumishi kutoka kwenye vituo vya utoaji wa huduma za chanjo ya kila siku na kila timu itakuwa na watoa huduma watatu ambao ni mchanjaji mmoja, mtunza takwimu mmoja, na mhudumu ngazi ya Jamii mmoja, pamoja na mhamasishaji' Amesema Bwisso.
Bwisso, amesema kuwa chanjo hiyo ya surua itahusisha watoto wa miezi 9 na chini ya miaka 4 na miezi 11, ambapo kwa Manispaa ya Morogoro jumla ya watoto 42000 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo.
Amesema kuwa chanjo hiyo itafanyika ndani ya siku 4 katika maeneo yao kama vile Mitaani, Sokoni, katika ofisi za Serikali, shuleni hasa katika shule za awali na Vituo vyote vya kulelea watoto.
Post a Comment