Header Ads

JIWA YAKABIDHI MSAADA WA VITU KWA WAHANGA WA MAFURIKO MANISPAA YA MOROGORO


KIKUNDI cha Wakina Mama cha Jiendeleza Women Association (JIWA) chenye makao yake Kihonda Maghorofani  Manispaa ya Morogoro, kimekabidhi vitu mbalimbali kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kwa ajili ya waathirika wa Mafuriko.

Misaada hiyo iliyotolewa na  JIWA Februari 07/2024,  inajumuisha  vyakula (unga Kg 175) , nguo mbalimbali, viatu vya wakubwa na watoto, pamoja na sabuni.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Mwenyekiti wa JIWA ,Bi. Doroth Lyoga,  amesema JIWA inaungana na familia za wahanga na kutoa misaada ya kibinadamu.

Lyoga, amesema msaada huo unalenga kutoa faraja na msaada wa msingi ili kusaidia katika kurejesha hali ya kawaida kwa wahanga wa mafuriko.

Aidha,amesema matarajio yao ni kuona familia duni ambazo zimeathirika sana ziweze kufikiwa na misaada hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, amekishukuru Kikundi cha JIWA, kwa kutoa msaada huo huku akisema kwamba  wataugawa kwa ufasaha ili uweze kuwasaidia wahanga  wa mafuriko.

"Nawashukuru sana , JIWA, wanawake ni Jeshi kubwa, hiki mlichokifanya ni taswira tosha kuwa mama ni mlezi na mama ndio muhimili wa familia, wenzetu wapo kwenye hudhuni, tukijitoa kama hivi tunawapa faraja kubwa sana, endeleeni na moyo huo huo lakini tunaomba Taasisi nyengine ziguswe na maafa haya ziige kama JIWA  wanavyofanya ya kuwakumbuka wenzetu walipatwa na maafa" AmesemaDC Nsemwa.

Kwa upande wa Mratibu wa Maafa Manispaa ya Morogoro, Elizabeth Badi,amekipongeza Kikundi cha wakina mama cha JIWA  kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii, hasa kwa wahanga wa mafuriko katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wakazi wamepoteza vitu na kuharibiwa miundombinu ya makazi.

Licha ya kukabidhi misaada hiyo, DC Nsemwa,amewaunga  mkono wakina mama hao kwa kununua bidhaa yao ya Siagi ya Karanga ambayo ni moja ya mradi ambao wakina mama hao wanafanya katika kuwaingizia kipato.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.