Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO KUENDELEA NA MAANDIKO 12 YA MIRADI YA MAENDELEO- ALLY MACHELA



MKURUGENZI wa  Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema Manispaa ya Morogoro inaendelea na maandiko 12  ya miradi ya maendeleo ikiwa na lengo la kuongeza mapato, kuboresha huduma bora kwa wananchi na kupendezesha Mji kuwa katika hadhi ya kisasa.

Hayo ameyazungumza Februari 19/2024  Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa Ofisi Kuu katika Kikao cha Kamati ya ushauri ya Wilaya (DCC) kilichoongozwa na Afisa Tarafa Manispaa ya Morogoro , Wifred Kipako, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa.

Machela, amesema hadi sasa maandiko ya miradi 4 yapo hatua za mwisho kukamilika kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na maandiko mengine yataendelea kuandikwa kwa mwaka ujao wa bajeti.

Kuhusu mapato ya ndani, Machela ,amesema makisio ya ndani ya mwaka 2024/2024 imepanda kwa asilimia 18.49 ukilinganisha na bajeti inayoendelea ya mwaka 2023/2024 ya mapato ya ndani ya shilingi 13,185,280,000.00  ambapo matarajio ya bajeti 2024/2025 ni kukusanya 15,622,877,022.00 ambapo shilingi 2,568,322,491.05 ni mapato lindwa na shilingi 13,054,554,531.00 ni mapato yasiyolindwa.

Hata hivyo , Machela, amesema Manispaa inategemea kutekeleza moja ya miradi ya kimkakati wa kujenga maghala 4 na maegesho ya Malori katika eneo la Kihonda Magereza ili kuendana na muingiliano sawa wa utoaji wa huduma zitakazoanza kutolewa na mradi wa Serikali Kuu wa treni ya mwendokasi (SGR).

Afisa Tarafa, Kipako, amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili taarifa mbalimbali zautendaji kazi wa halmashauri na taasisi zote zilizopo ndani ya Manispaa ya Morogoro.

Katika kikao hicho, Wajumbe wa kamati hii walipata wasaa wa kujadili na kupitisha taarifa hizo ambapo kwa ujumla wake hali ya utendaji kazi wa taasisi hizo ni nzuri,  aidha shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika taasisi mbalimbali unaendeleavizuri.

Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Dkt. Abdulaaziz Abood, ameshauri kwamba halmashauri ihakikishe katika Vituo vya kutolea huduma viwe na wahudumu wa kutosha ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya.

Mhe. Abood, pia ameshauri wakati wa ujenzi wa miradi ya maendeleo, Halmashauri ihakikishe kuwa inakamilisha miradi yote bila viporo.

"Kama tumeamua kujenga shule, tukamilishe kila miundombinu inayotakiwa kuliko kuwa na miradi mingi harafu tunakuwa na viporo vya miradi ambayo tumeianzisha, kama ni shule jenga shule, kamilisha vyoo na huduma zote kisha tuhame kwenye mradi mwengine" Amesema Mhe. Abood.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Christine  Ishengoma, ameitaka Halmashauri kuhakikisha inatupia macho kwa upana wake barabara za pembezoni kwani asilimia kubwa ya barabara hizo ni changamoto kwa wananchi.

Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mohamed Lukwele, amesema ushauri ambao umetolewa na wadau  wanauchukua na yale ambayo ytahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka watayafanya lengo ni kuona wanchi wa Manispaa ya Morogoro wanapata huduma bora.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.