Header Ads

WAZEE 468 KATA YA UWANJA WA TAIFA WAPATIWA BIMA ZA AFYA CHF KUPITIA UFADHILI WA WEZESHA MABADILIKO



JUMLA ya Wazee  468 Kata ya Uwanja wa Taifa Manispaa ya Morogoro  wamepatiwa kadi za bima ya afya ya jamii (CHF) .

Zoezi la kugawa bima hizo limefanikiwa kugusa jumla ya Kaya 78 , limefanyika  Februari 22/2024 kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Kata ya Uwanja wa Taifa.

Akiongea kwenye zoezi hilo,Diwani wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Mhe.Majuto Mbuguyu akiwa mgeni rasmi, amempongeza Diwani wa Kata ya Uwanja wa Taifa Mhe. Rashid Matesa pamoja na mfadhili wa bima hizo Mkurugenzi wa Taasisi ya Wezesha Mabadiliko, Dkt. Lusako Mwakiluma kwa  kuwapa vitambulisho na kuwalipia wazee bima ya afya.

“Nawapongeza kwa hatua hii,  nyie mmejiongeza, maana hamkuwapa wazee vitambulisho tuu, bali na kuwalipia kabisa bima ya afya ili kuweza kupata huduma za afya bila ya malipo, Mhe. Matesa natambua uwezo wako ulionao katika Uongozi endelea na moyo huo huo wa kuhaakikisha unagusa matatizo ya wananchi wako " Amesema Mhe. Mbuguyu.

Akiongeza juu ya kuwalipia wazee kadi ya bima ya afya, Diwani wa Kata ya Uwanja wa Taifa, Mhe. Rashid Matesa, amemshukuru Dkt. Mwakiluma, na timu yake ya Wezesha Mabadiliko  kwa kuwajali wazee wa Kata hiyo.

Matesa, amesema bima hizo ni awamu ya kwanza lakini lengo ni kila mzee  katika Kata hiyo anatakiwa apewe bima ya afya.

“Kwa kuwa na kadi ya bima ya afya kunamfanya mzee huyu kupata huduma zote za afya bure na bila ya kuwa na ule usumbufu wa kwenda kwa Mtandaji wa Kata na Mtendaji wa Mtaa ili aandikiwe barua, tunayo Zahanati yetu ni muda wenu wazee kwenda na kadi zenu kutibiwa, Serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali wazee ndio maana kuna vitambulisho vya kadi ya masamaha wa matibabu kwa wazee " Amesema Mhe. Matesa.”

Naye Katibu wa Baraza la Wazee Manispaa ya Morogoro, Dkt. Bakili Anga, amempongeza Diwani na mfadhili kwa kuwawezesha wazee huduma hiyo muhimu ambayo itakuwa mkombozi kwa wazee kupata huduma za afya bila malipo.

Dkt. Anga, amesema licha ya mdau kujitokeza kulipa bima za wazee, ameomba zoezi la kuwapa wazee vitambulisho  vya matibabu bure liende kwa kasi kwani agizo hilo lilitolewa na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Kupitia agizo hilo Halmashauri zinatakiwa kuwapa wazee vitambulisho vya matibabu bure wazee wote wasio na uwezo ili kuwaondoshea usumbufu wanapokwenda hospitali kutibiwa.

Wakiongea kwa nyakati tofauti tofauti,  baadhi ya wazee waliopata kadi ya bima ya afya, wamemshukuru Diwani  , timu yake ya BMK pamoja na mfadhili  kwa kuwaangalia kwa jicho la huruma na hakika wanaona Serikali yao bado inawajali na kuwathamini.

“Mjukuu wangu, kwa umri wetu huu magonjwa ndio nyumbani kwake, sasa kama huna pesa na huna namna ya kupata matibabu hapo inakuwa mtihani. Japo suala la kufa ni ahadi ya Mwenyezi Mungu lakini kukosa matibabu kunachangia vifo vya haraka kwetu sisi wazee” Amesema  mmoja ya wazee hao.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.