Header Ads

VIONGOZI WA DINI WATAKIWA KUHAMASISHA WANANCHI UTUNZAJI WA MAZINGIRA


MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa, ametoa wito kwa viongozi wa dini kuhamasisha jamii umuhimu wa kuhifadhi  mazingira.

Kauli hiyo ameizungumza Aprili 29/2023 katika zoezi la upandaji wa miti Bwawa la Mindu Manispaa ya Morogoro  lililoandaliwa chini ya uratibu wa Balozi wa Mazingira Ofisi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Chage Alex Chage.

Akizungumza na wadau wa Mazingira waliojitokeza katika upandaji wa miti , RC Mwassa, amesema kufanya hivyo ni kutimiza matakwa ya sheria  ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 ambayo  imeweka wazi. misingi ya jumla katika suala zima  la uhifadhi  wa mazingira.

RC Mwassa, amesema kuwa viongozi  wa dini wanao wajibu  wa kuhakikisha  wanaendelea  kutoa elimu kupitia mafundisho  ya dini juu ya kutimiza  matakwa  ya sera  ya mazingira  ya mwaka 2021 ili malengo yaliyowekwa na serikali katika sekta ya uhifadhi mazingira yanatimia na Tanzania  inakuwa mstari wa  mbele  katika kukabiliana  na mabadiliko ya tabiachi.

Kwa upande Mgeni rasmi katika zoezi hilo la upandaji wa Miti, Askofu wa Kanisa la KKKT-Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameyo , ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa dini  kuhakikisha wanaendelea na  utunzaji wa mazingira kwani mazingira yasipotunzwa yanaweza kuleta majanga  kama vile ukame,mafuriko na kwamba majanga hayo hayachagui dini bali yanakuja kwa wote. 

Naye Mratibu wa Kampeni hiyo ya upandaji wa Miti ambaye pia ni Balozi Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,  Chege Alex Chage, amesema kuwa suala la Utunzaji wa Mazingira ni Wajibu wa kila Mmoja wetu katika jamii kushirikiana na sekta  Binafsi pamoja na Serikali kwa ujumla .

Chage, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa, kwa usimamizi mkubwa wa utunzaji wa mazingira, pamoja na wadau wote wa Mazingira ambao amekuwa akiungana nao kila anapofanya Kampeni zake ambazo zimekuwa zikitumika kumsaidia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jaffo kwa ajili ya kutimiza wajibu wake.

"Kwa mkoa wetu na Taifa kwa ujumla tumekuwa na kampeni nyingi za Mazingira, tumeanza na wanafunzi kwa kuwa na Kampeni ya Soma na Mti, lakini kwa wananchi nako Ishi na Mti, hizi ni kampeni zenye kulenga uhifadhi wa Mazingira kwa kupanda miti,mimi kwa nfasi ya Ubalozi kazi kubwa ni kumsaidia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jaffo kwa ajili ya kutimiza wajibu wake pamoja na kuona Tanzania yetu tuna rudisha Uoto wa asili katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi" Amesema Chage.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.