Header Ads

BMK MAFIGA YAKABIDHI MIRADI YA MADARASA NA MAKTABA VYENYE THAMANI YA MILIONI 150 KWA KAMATI YA SIASA YA KATA.



BARAZA la Maendeleo Kata ya Mafiga chini ya Mwenyekiti wake ambaye ndiye Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Thomas Butabile, wamekabidhi miradi ya shule ikiwemo Maktaba ya Shule ya Sekondari Mafiga pamoja vyumba vipya vya madarasa Shule ya Msingi Mafiga B.

Akizungumza katika mapokezi hayo ya miradi hiyo, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Kata ya Mafiga, Ndg. Juma Habibu, amesema, wao kama wasimamizi wa Ilani ya Chama, wameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kubariki kuendelea kutumika kwa ajili ya kutoa huduma.

Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ,Ally Machela, kwa kushirikiana na timu ya Wataalamu kwa kuitekeleza vizuri ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo.

Hata hivyo, amempongeza Diwani wa Kata ya Mafiga Mhe. Thomas Butabile na timu yake ya BMK  kwa ushirikiano  wao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuweza kuifanya  Mafiga  iwe na ongezeko la kimaendeleo.

Naye Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile, amesema katika ujenzi wa madarasa hayo mapya shule ya Msingi Mafiga B, Ofisi ya Kata ilipokea shilingi Milioni 67,376,180.00  na kupokea tena milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya Maktaba Shule ya Sekondari Mafiga.

Aidha, Mhe. Butabile, amesema hadi kukamilika kwa majengo hayo kutasiaidia kuimarisha huduma za elimu na ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi.

Amesema kuwa katika madarasa ya Shule ya Msingi Mafiga B,  zaidi ya milioni 67,376,180 zimetolewa na Ofisi ya Mkurugenzi  zimetumika katika ujenzi huo ambapo ujenzi wa jumla umegahrimu milioni 109,170,410.00 ambapo shilingi milioni 40,775,880.00 ni fedha za nguvu ya wananchi na wadau wa maendeleo, milioni 2,244,200.00 michango ya wazazi wa wanafunzi wa shule hiyo.

Butabile ,amesema kukamilika kwa mradi wa madarasa kutasaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi darasani, kuongeza ari ya wanafunzi na waalimu katika ufanisi wa kujifunza, pamoja na kuongeza ufaulu shuleni kutokana na mazingira rafiki ya kujifunzia.

Hata hivyo,amesema safari haijaishia hapo kwani mpango uliopo ni kuhakikisha wanakwenda kukamilisha ujenzi wa madarasa 3  na Ofisi katika Shule ya Msingi Misufini B  , Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata, nyumba ya mwalimu wa shule ya Msingi Mafiga B , Maabara ya Kituo cha afya cha Mafiga ambapo miradi yote hiyo inasubiri fedha za umaliziaji kutoka Halmashauri.

Upande wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mafiga, Amina Saidi, amewapongeza wazazi pamoja na wadau wa maendeleo kwa kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo mapya huku shukrani za kipekee akizielekeza kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kutoa fedha hizo za ujenzi wa madarasa.

"Ujenzi huu hatujaufanikisha peke yetu, tunakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kusimamia vyema Ilani ya Chama , namshukuru Diwani wetu kwa kuwa bega kwa bega usiku na mchana, nawashukuru sana watendaji wenzangu, wazazi, wadau wa maendeleo wakiwemo wafanyabiashara wa ndani na nje ya Kata yetu, Viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kujitoa kwa hali na mali katika kufanikisha ujenzi unafikia hatua ya kupata fedha za umaliziaji" Amesema Amina.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.