Header Ads

WATENDAJI WA MITAA WATAKIWA KUSIMAMIA VYEMA MKATABA WA LISHE


WATENDAJI wa Mitaa Manispaa ya Morogoro  wameagizwa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa viashiria vyote vilivyomo katika mkataba wa lishe ili kuleta mabadiliko katika kuboresha hali ya lishe kuanzia ngazi ya kaya hadi jamii nzima pamoja na kuweka utaratibu maalum wa kuadhimisha siku ya lishe kwa kila kata.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro,  Jacqueline Mashurano, katika kikao kazi na Maafisa Watendaji wa Mitaa juu ya kukumbushana viashiria vya mkataba wa lishe ngazi ya Mitaa ,katika ukumbi wa Mikutano wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro Aprili 20/2023.

Akizungumza na Watendaji hao wa Mitaa, Mashurano, ameeleza kuwa viashiria vinavyotakiwa kutekelezwa ni pamoja na Watoto kupatiwa chakula mashuleni, wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ipasavyo na kupatiwa madini joto, Watoto kupatiwa vitamin A, Watoto wenye utapiamlo mkali kupatiwa huduma vituoni na utoaji wa fedha ipasavyo kwa ajili ya afua za lishe.

“Watendaji wote hakikisheni mnasimamia vigezo vya upimaji na vipaumbele vya viashiria vya lishe, na muhakikishe kuwa mnapata  taarifa za hali ya lishe kwa Watoto chini ya miaka mitano, kufanya ufuatiliaji wa Watoto walioacha matibabu ya utapiamlo kwa kushirikiana na watoa huduma za afya ngazi ya jamii.” Amesema Mashurano.

Mashurano, amesema kuwa ataendelea kujipanga Zaidi ili kuhakikisha kata zote ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kila kiashiria kinafika asilimia 95 na sio chini ya hapo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wazazi watambue umuhimu wa kuchangia chakula cha Watoto mashuleni ili kukuza kiwango chao cha lishe, kuongeza usikivu na kupunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi.

Naye Mratibu wa iCHF iliyoboreshwa Manispaa ya Morogoro, Saada Mustapha, amesema yapo maagizo ya iCHF ambayo Watendaji wa Mitaa wanatakiwa kuyafanya katika maeneo yao ya kazi.

Miongoni mwa maagizo hayo ni pamoja na kuhamasisha jamii ili kuweza kujiunga na bima ya afya iliyoboreshwa, kufikia lengo la asilimia 10 ya uandikishaji kwa kila Kata/Mtaa.

Kwa upande wa Mratibu wa mradi wa Lishe Endelevu Mkoa wa Morogoro, Mariam Mwita, amesema suala la lishe ni mtambuka hivyo jamii kwa kushirikiana na wadau mbali mbali pamoja na Serikali kuhakikisha wanajenga Vizazi vyenye watoto wenye afya na lishe bora ili kuepuka udumavu.

Utekelezaji wa mkataba wa lishe uliosainiwa utakuwa wa miaka nane kuanzia tarehe mosi Julai 2022 hadi tarehe 30 Juni 2030 kulingana na malengo na shabaha zilizoainishwa katika mikakati ya kitaifa ya muda mfupi, muda wa kati pamoja na muda mrefu ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka  2025, mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala na Sera mbalimbali za nchi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.