Header Ads

RAIS SAMIA AWATAKA WAFANYAKAZI KUWA WAADILIFU, KUFANYA KAZI KWA WELEDI.

RAIS  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wafanyakazi wa Sekta zote hapa nchini kufanya kazi kwa Weledi na kuwa waadilifu katika utendaji wao kazini.

Rais Samia ameyasema hayo Mei 1 mwaka 2023, wakati akihutubia Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo Kitaifa yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.

Dkt. Samia amesema pamoja na Wafanyakazi hao kudai maslahi yao ya kazi bado wanatakiwa kuwa  waadilifu na kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza majukumu yao.

“kwa hiyo pamoja na kudai mishahara bora, lakini uadilifu na weledi kazini ndio utaleta maisha bora kwa wafanyakazi...”. Amesema Rais Samia.

Sambamba na hilo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wafanyakazi kuwa Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo, kuwapandisha madaraja wafanyakazi, kuwaongezea mishahara na posho za wafanyakazi.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema kutakuwa na nyongeza za mishahara kwa wafanyakazi ambayo itakuwa inaongezeka kwa kila mwaka, nyongeza hiyo inatarajia kuanza mwaka huu 2023.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa wakati akitoa salam za Mkoa, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa zinazofanywa katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mhe. Fatma Mwassa ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia wafanyakazi Mkoani Morogoro wameboreshewa maslahi yao ikiwemo kupandishwa madaraja takribani wafanyakazi 7108 wamepandishwa madaraja, 2030 wameajiriwa kwa sasa Mkoa umepata kibali cha kuajiri wafanyakazi 3891 wa kada mbalimbali pamoja na kuongeza mishahara.

Nae Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya ameishukuru Serikali sikivu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali wafanyakazi wake kwa kuwaboreshea mazingira na maslahi yao ya kazi, kulipa2 madai yao, kupandisha vyeo watumishi, pamoja na kuwaongezea mshahara.

Maadhimisho hayo ya Mei Mosi kwa Mwaka huu yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Mishahara bora na ajira ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi, wakati ni sasa”.



No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.