Header Ads

JUMUIYA YA AHMADIYYA MOROGORO YATOA MSAADA WA VYAKULA KWA ZAIDI YA KAYA 150 ZENYE UHITAJI.



JUMUIYA ya Kiislamu ya Ahmadiyya Morogoro imetoa msaada wa vyakula kwa zaidi ya  Kaya 150 zenye uhitaji kutoka Mitaa ya Ngerengere, Kitata, Msamvu B, Mtaa wa Mbuyuni pamoja na Mtaa wa Airport iliyopo  Kata ya Kihonda Maghorofani Manispaa ya Morogoro ikiwa ni chakula kwa ajili ya Mkono wa Eid Fitri ambapo utaratibu huo umekuwa ukifanyika kabla ya Sikukuu.

Hafla hiyo fupi ya ugawaji wa vyakula imefanyika Aprili 13/2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ahmadya Kihonda Maghorofani.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la ugawaji wa vyakula,Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ambaye ndiye mgeni katika hafla hiyo, ameushukuru Uongozi wa Ahmadyya, kwa kujitoa kwao hususani katika kutoa huduma ya elimu kwa kuwa na shule zao, huduma ya afya katika Hospitali zao pamoja na kutoa huduma ya kiroho.

Kauli hiyo ameitoa Aprili 13/2023 katika kugawa chakula kwa wahitaji zaidi  katika Mitaa 5 ya Kata ya Kihonda Maghorofani chakula kilichoandaliwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Ahmadyya Muslim Jamaat.

"Wenzetu Ahmadyya licha ya kugawa zawadi hii ya Mkono wa Eid ya vyakula lakini wanatukumbusha kuwa na upendo pamoja na kusaidiana, hili sio jambo dogo , ni jambo la kiimani lenye kumpendeza Mwenyezi Mungu, ukiwa na roho ya uchamungu hata mambo yako yanafanikiwa, tumeona rushwa, uongo , dhuruma, ufisadi , ulawiti haya yote ni matokeo ya kutokuwa mchamungu na kukosa hofu ya Mungu" Amesema RC Mwassa.

RC Mwassa, amewataka wazazi kuhakikisha watoto wanawalea katika maadili ya kumcha Mungu ili kuweza kuwa na Viongozi watakaoongoza Tanzania katika imani na misingi ya Kimungu.

Aidha, RC Mwassa, amewataka Wazazi kujitoa  katika kujifunza jinsi ya kuwalea watoto katika misingi halisi ya kumjua Mungu.

Naye Mkuu wa Chuo cha Jumuiya ya Ahmadiyya Morogoro, Sheikh Abid Mahmood Bhatti, amesema kuwa  msaada huo umetolewa kuunga mkono wito wa serikali inayohimiza mashirika,taasisi,na watu binafsi kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji.

Bhatti, amesema licha ya kuunga mkono Serikali  lakini pia kuweza kutoa zakatul Fitri kwa jamii ili kuweza kujumuika na jamii katika kusherehekea Sikuu ya Eid Fitr.

"Jumuiya ya Ahmadiyya ni moja ya sehemu inayojihusisha na utoaji wa misaada mbalimbali ikiwemo ya kiafya,kielimu na kijamii kwa kuwafikia watu wenye uhitaji, hivyo kutoa kwetu chakula kwa watu wenye uhitaji kwanza tumetekeleza misingi ya dini , kwani sisi tumekuwa tukifanya hivi kila ifikapo Siku ya Eid basi tumekuwa tukijumuika na ndugu zetu kuhakikisha kwamba tunakuwa nao pamoja katika kusheherekea sikukuu hii " Amesema Bhatti.

Miongoni wa vyakula hivyo vilivyo gharimi takribani Shilingi Milioni 3 na zaidi, ni  pamoja na Mchele mfuko wenye  Kilo 5 na Unga wa Sembe Mfuko wa Kilo 10.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.