MASHEKHE NA MAIMAMU WATAKIWAKUHIMIZA UMOJA NA MSHIKAMANO.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa amewataka Mashekhe na Maimamu wa Misikiti ya Mkoa wa Morogoro kuhimiza waamini wao na wananchi wa Mkoa huo kwa ujumla kudumisha umoja na mshikamano, zaidi kuhimiza amani na watu kuwa na hofu ya mungu kwa kufanya hivyo amesema kutapunguza maovu mengi yanayotokea ndani ya jamii ya leo.
Mhe. Fatma Mwassa ameyasema hayo Machi 26 mwaka huu wakati wa hafla fupi ya kutoa sadaka ya futari kwa Mashekhe na Maimamu wa Misikiti ya Morogoro Mjini iliyofanyika Ofisini kwake.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema jamii ikiwa na hofu ya Mungu maovu yanapungua, hivyo amewataka viongozi hao kutumia mfungo huu wa Ramadhani kuwahimiza waumini wao kuwa waadilifu na kuacha matendo yote yasiyofaa katika jamii.
"...kwahiyo niwaombe sana kutumia kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwahimiza waumini wenu kuwa watu waadilifu, na kuacha uharifu, kuacha wizi, uzinzi, rushwa na mambo mengine yote mabaya..." amesema Mhe. Fatma Mwassa.
Sambamba na hilo Mhe. Fatma Mwassa amewataka kwenda kuwahimiza amani, upendo, umoja na mshikamano baina ya watanzania wote.
Kwa upande wake Katibu wa Bakwata Mkoa wa Morogoro Shekhe Kindo Mbagu kwa niaba ya Mashekhe na Maimamu waliopokea sadaka hiyo amemshukuru na kumuombea dua Mkuu huyo wa Mkoa kwa kuwakumbuka Mashekhe na Maimamu ambao mara nyingi hawafikiwi.
Aidha, ameongeza kuwa wataendelea kuwahimiza waumini kudumisha amani, upendo na mshikamano kwa kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae Alhaji Khamis Sengulo ambaye ni Mjumbe wa Baraza kuu la BAKWATA Mkoa wa Morogoro amesisitiza kuwa kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kutoa kwa wahitaji, mwezi wa kudumisha upendo, umoja na amani pamoja na kufanya ibada kwa wingi, hivyo Waislamu wanatakiwa kutoa kama alivyofanya Mkuu wa Mkoa Mhe. Fatma Mwassa
Katika hafla hiyo Mkuu huyo wa Mkoa ametoa chakula kama mchele, tende, mafuta ya kula, sukari, tambi, mikeka ya kuswalia na masaafu ikiwa ni ishara ya matendo mema yanayotakiwa kutendwa zaidi katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Post a Comment