DC NSEMWA AFUTURISHA, AHIMIZA WANANCHI KUDUMISHA AMANI NA UPENDO.
MKUU wa Wilya ya Morogoro, Mhe.Rebecca Nsemwa, amewataka Wananchi hususani wa Wilaya ya Morogoro, kuendelea kudumisha upendo, umoja na mshikamano ikiwemo kufanya kazi kwa bidii.
Kauli hiyo ameitoa Aprili 18/2023 katika Ukumbi wa DDC Mbaraka Mwinshehe wakati wa hafla fupi ya kufuturisha wananchi pamoja na waumini wa Kiislamu .
Akizungumza na Wananchi hao waliojitokeza katika iftari hiyo, DC Nsemwa,amewataka wananchi kudumisha amani na upendo huku akiwasititiza kuachana na tabia ya ubaguzi.
DC Nsemwa, amewapongeza Wananchi wote waliojitokeza katika iftari hiyo aliyoiandaa , huku akiahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Dini zote katika kudumisha amani na upendo na kuwaletea wananchi maendeleo.
Hata hivyo, DC Nsemwa, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, dini na wanachi kwa ujumla kudumisha amani na utulivu uliopo bila kujali tofauti za itikadi zao, dini au makabila yao.
“mashujaa wetu wakati wakiipigania amani ya nchi yetu hawakuangalia vyama vyao, wala dini zao, walichojali ni utanzania wao na ndiyo amani tunayojivua hadi hii leo, hivyo naomba amani tuliyonayo Watanzania tusiitie doa, tuendelee kuing'arisha kwa upendo wetu na mshikamano wetu "Amesema DC Nsemwa.
Pia ametaka kuwe na vyombo vya kuleta matumaini kwenye jamii badala ya kukatishana tamaa na kukimbilia mambo yanayoashiria uvunjifu wa amani.
Aidha, DC Nsemwa , ametuma salamu ya heri ya Sikuuu ya Eid kwa wananchi wote na waumini wa Kiislamu wa Wilaya ya Morogoro, huku akiwaomba waendelee kufuata misingi ya dini na kudumisha upendo katika kuendelea kuiweka Wilaya ya Morogoro katika taswira nzuri pamoja na kuleta maendeleo na ustawi kwa taifa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Machela, amewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa atasimamia kwa nguvu zote masuala yote yanayohusu maendeleo ya Manispaa ya Morogoro ikiwemo kudumisha mshikamano , upendo na amani kwa faida ya wananchi wote wa Manispaa ya Morogoro.
Machela , amesema kuwa sehemu ambayo hakuna amani basi hata utulivu wa maendeleo unakosekana.
Aidha, amesema kuwa amefurahishwa sana na mshikamano wa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kwa kuwa na dhamira ya pamoja ya kujadiliana mambo yenye maslahi mapana ya Manispaa ya Morogoro kwa kusimamia kikamilifu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020-2025.
Post a Comment