MAMA MAKINDA AWATAKA WATANZANIA WATAMBUE UMUHIMU WA SENSA .
KAMISAA wa Sensa , na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mama Anna Makinda, amewataka Watanzania watambue umuhimu wa zoezi la Sensa na kuanza kujiandaa kwa kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Hayo ameyasema Septemba 01/2021 katika Mkutano wa Sensa ya Majaribio iliyofanyika Mtaa wa Mtawala Kata ya Mwembesongo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mama Makinda, amesema Sensa ya Majaribio ni moja ya mpango ambao Serikali imeuweka ili kuona jinsi Sensa ya Mwakani itakavyoweza kufanyika na kufanikiwa hukuakiwaomba Watanzania watambue umuhimu wa zoezi hilo na kuanza kujiandaa kwa kuhesabiwa kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa.
" Lengo la sensa ya watu na makazi ni kuiwezesha serikali na jamii kwa ujumla kuweka misingi ya kutunga sera ambazo zinatafanikisha maendeleo kwa Taifa na watu wake, hivyo ni vyema Wananchi wakalichukulia suala hili kwa uzito na umuhimu mkubwa , tunaamini Sensa ya Mwaka huu kuna mabadiliko makubwa yatatokea kikubwa ni ushirikiano wa Wananchi " Amesema Mama Makinda.
Mama Makinda amesema kuwa , mara baada ya kukamilika kwa sensa ya majaribio wanatarajia kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili kujadili changamoto zilizojitokeza na kuboresha kwa ajili ya sensa ya mwakani.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk. Albina Chuwa, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa sensa ya watu na makazi Ofisi yake imedhamiria kuboresha zoezi hilo la Sensa ya majaribio ili kuweza kurekebisha kasoro zinazoweza kujitokeza hapo baadae.
Dk. Chuwa , amesema kuwa katika sensa ya majaribio jumla ya kaya 5000 zitahojiwa kwa ajili ya kupata taarifa zao muhimu ambazo zitaingizwa katika kumbukumbu za NB.
Hata hivyo, Dk Chuwa, amesema kutokana na hali hiyo NBS itatoa mafunzo kwa watu wapatao 100, 000 kwa ajili ya kukusanya taarifa kwa namna itakayokidhi vigezo na mfumo thabiti wa mafunzo kwa watalaamu wake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amesema kwa kutambua muhimu wa sensa serikali imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha sensa ya watu na makazi inafanikiwa kwa ubora wa hali ya juu ili kwenda sambamba na mafanikio ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania.
Hata hivyo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, amesema kuwa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kwa kuhsirikiana na Wananchi watahakikisha zoezi hilo linafanikiwa na linaleta matokeo chanya.
" Mimi nikiwa mwakilishi wa Madiwani wa Manispaa ya Morogoro, tutashirikiana vyema na wananchi ili kutoa ushirikiano na kuwezesha zoezi la Sensa linafanikiwa, tunatambua umuhimu wa Sensa kwani hata sisi katiika Bajeti zetu tukiwa na takwimu sahihi itatusaidia kuweka vipaumbele vyetu kwa wananchi wetu" Amesema Mhe. Kihanga.
Post a Comment