MACHINGA SHIUMA TAIFA WAPONGEZA UONGOZI WA SERIKALI MKOA WA MOROGORO KWA JITIHADA ZA KUWAJENGEA MAZINGIRA RAFIKI MACHINGA.
Viongozi wa SHIUMA Taifa , wakiwa pamoja na Viongozi wa SHIUMA Manispa ya Morogoro na machinga wakiwa katika picha ya pamoja.(wa sita kulia waliosimama mbele Katibu wa SHIUMA Taifa, Ndg. Venatus Anatory).
Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa, Ernest Masanja, akizungumza na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Machinga Manispaa ya Morogoro Juma Shaibu Ndeka,akizungumza na waandishi wa habari.
SHIRIKISHO la Umoja wa Machinga Taifa (SHIUMA) umeupongeza Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro kwa usimamizi mzuri na kuwajengea mazingira rafiki Machinga katika kufanya kazi zao za kuingiza kipato.
Kauli hiyo ya pongezi imetolewa leo Septemba 06/2021na Mwenyekiti wa SHIUMA Taifa katika Mkutano wa waandishi wa habari na wamachinga uliofanyika Katika Ukumbi wa Mikutano wa Kingo Manispaa ya Morogoro Soko Kuu la Chifu Kingalu.
Akizungumza na Waandishi wa habari kwa niaba ya Wamachinga SHIUMA Taifa , Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Ndg. Ernest Masanja, amesema Viongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Viongozi wa Wilaya na Halmashauri wamefanya kazi kubwa katika kusimamia utaratibu mzuri wa kuwapanga na kuwajengea machinga mazingira rafiki ya kufanya shughuli zao.Masanja, amechukua nafasi ya Kumpongeza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, kwa kuwa karibu nao na kuwashirikisha kwa kila jambo kitu ambacho kinawajengea faraja Wafanyabiashara na kuona Serikali inawaunga mkono kama alivyotamka Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwataka Wamachinga kufanya biashara zao bila ya kubugudhiwa.
"Mkuu wa Wilaya Kaka yangu, Albert Msando, tunakushukuru sana pamoja na Uongozi wako wa Wilaya, umekuwa msaada mkubwa sana kwa upande wetu, umesimama mstari wa mbele kuhakikisha maslahi ya Wamachinga unayasimia kikamilifu, pia tumeona Manispaa inabadilika , miradi mikubwa mnayoitekeleza kwakweli inatupa faraja sana sisi wana Morogoro, kwani tunaamini baada ya kukamilika miradi hii Manispaa tutakuwa tuna vyanzo vizuri vya kukusanya mapato yetu ya ndani na kutengeneza miradi mingine kwa lengo la kuwahudumia Wananchi, nichukue nafasi hii kusema tunaomba usituchoke kaka yetu tunapopatwa na changamoto zidisha nguvu zako za kutukwamua" Amesema Masanja.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Machinga Manispaa ya Morogoro Juma Shaibu Ndeka , amechukua nafasi hiyo kwa kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Ally Hamu Machela , huku akisema wapo tayari kumpa ushirikiano wakutosha kwani lengo lao sio kubaki nyuma ni kusonga mbele.
"Tunapenda kumkaribisha Mkurugenzi wetu katika Manispaa yetu, tunamhakikishia tutakuwa nae bega kwa bega na taarifa zozote atakazo zihitaji tutampatia lengo ni kuijenga Manispaa yetu isonge mbele na wamachinga wasonge mbele, tunamuomba kwa muda wake tuweze kuonana naye sisi viongozi na tuanze kumpatia maelezo juu ya Chama chetu, mikakati , mafanikio pamoja na changamoto ziazotukabili," Amesema Ndeka.
Post a Comment