Header Ads

KAMATI YA FEDHA NA MIPANGO YAZIAGIZA KAMATI ZA USIMAMIZI WA MIRADI KUSHIRIKIANA KAKAMILISHA MIRADI KWA WAKATI.

 

KAMATI ya Fedha na Mipango Manispaa ya Morogoro ikiongozwa na Mwenyekiti hiyo ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga, imewaagiza wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha wanasimamia  vizuri na kwa haraka zaidi na kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja kama kamati kutatua changamoto zozote zitakazo wakabili katika utekelezaji wa mipango yote iliyowekwa katika ukamilishaji wa miradi hiyo.

Kauli hiyo ,imetolewa Septemba 06/2021 , wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Manispaa ya Morogoro.

Akizungumza juu ya kamati za usimamizi wa miradi, Mhe. Pascal  Kihanga, amesema kuwa kama kamati za usimamizi wa miradi zitashirikiana  kwa pamoja basi miradi yote inayotekelezwa itamalizika kwa wakati.

Kihanga, amewaomba  Wajumbe  wa Kamati hiyo kuweza kukagua na kutoa mapendekezo ya Miradi ya Maendeleo inayo tekelezwa na Halmashauri kwa kipindi husika pamoja na kushauriana juu ya utekelezaji wa miradi hiyo  ambapo  moja ya jukumu kubwa ni kuhakikisha kamati inakagua  eneo husika kwa wakati ili kutambua changamoto zilizopo na kutafuta njia mbala za kuweza kutatua changamoto hizo kwa wakati.

Aidha katika ukaguzi wa shule ya Msingi Jitegemee iliyopo Kata ya Chamwino , kamati imekubaliana kwa kufuata taratibu bila kuathiri sehemu yoyote kubomoa Shule hiyo kisha kutafuta eneo lingine ambalo wanaweza kujenga Shule mpya kwa ajili ya wanafunzi ambao walikua wakisoma hapo kutokana na majengo ya shule hiyo kuharibika sana.

Katika kukagua Shule ya Msingi Lukobe wajumbe wa kamati ya fedha wamempongeza Mkuu wa Shule hiyo kwa Uongozi mzuri katika usimamizi wa mradi huo ikiwemo Matundu Nane ya Vyoo na Madarasa mawili na kutaka wawasilishe changamoto zinazo wakabili katika utekelezaji wa mradi huo ili zitatuliwe na uweze kukamilika kwa haraka zaidi.

Katika ziara hiyo, Kamati  imefanya ukaguzi katika Shule ya sekondari Kilakala ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Ukumbi wa Shule hiyo  ambao una uwezo wa kuingiza watu Mia nne (400) ambapo kwa sasa ujenzi huo upo katika hatua nzuri ya utekelezaji.

Mbali na mradi huo wa ujenzi wa Ukumbi wa Shule ya Sekondari Kilakala, Kamati wametembelea  Shule ya Msingi Kingolwira kukagua Ujenzi wa Uzio unaoendelea katika shule hiyo ambao mazingira yanayoizunguka shule hiyo yanaweka hatarini usalama wa wanafunzi wanaosoma hapo.   

"Ujenzi wa Uzio huu utasaidia sana kuwaweka salama watoto wetu pindi wanapokuwa hapa kwa ajili ya masomo, kwa sababu ukiangalia mazingira ya Shule hii kwa watoto wadogo kama hawa ni hatari sana, hivyo inabidi ujenzi huu ukamilike haraka sana ili kuwaweka watoto wetu salama zaidi" Amesema Mh. Kihanga.

Kamati hiyo katika ziara yake ya Septemba 06/2021 Kamati  imetembelea Shule za Msingi ikiwemo Shule ya Msingi Lukobe, Kingolwira, Jitegemee na Ujenzi wa Shule mpya ya ghorofa Boma pamoja na kufanya ukaguzi  wa eneo la Ujenzi wa Hospitali ya wilaya Mkundi.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.