Header Ads

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAPONGEZA MANISPAA YA MOROGORO KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO.

 

 

HALMASHAURI ya mji Kibaha imetoa pongezi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya Wananchi wa Manispaa hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa Septemba 23, 2021 wakati wa ziara ya kamati ya fedha ya Halmashauri ya Mji Kibaha ndani  ya Manispaa hiyo kwa ajili ya kujifunza miradi mikubwa ya maendelea ikiwemo Soko kuu la Chifu Kingalu na  stendi ya Mabasi ya Msamvu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe. Mussa Ndomba amesema kuwa kitendo cha Manispaa ya Morogoro kutekeleza miradi ya maendeleo ni moja ya hatua kubwa ya kuhakikisha ya kwamba wananchi wanapata huduma bora

“Tunawapongeza sana Manispaa ya Morogoro kwa kutekeleza miradi hii mikubwa ya maendeleo, soko kuu pamoja na kituo cha mabasi cha kisasa Msamvu ni hatua kubwa mno mmeifanya, tumeona mmefanikiwa jinsi ya kuwapanga wafanyabiashara wadogo wadogo, sisi tumekuja kujifunza kutoka kwenu na tunakwenda kutekeleza katika Halmashauri yetu.” Amesema Mhe. Mussa.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kwa mwaka Manispaa ya Morogoro inakusanya zadi ya Bilioni 11 , hivyo kuongezeka kwa vitega uchumi vitasaidia kuongeza Zaidi pato la Manispaa.

“Sisi tumewatangulia, tunaamini kujifunza kwenu hapa, mnaweza nyinyi mkafanya vizuri Zaidi yetu sisi, Manispaa yetu ni chuo cha kujifunzia kwahiyo ujio wenu kwetu unatufanya na sisi tuongeze nguvu katika kutafuta vyanzo vyengine vya mapato” Amesema Mhe. Kihanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha,Msham Mbunde,ameongeza kuwa Manispaa ya Morogoro ina vitega uchumi vingi na kutokana na kujifunza vitega uchumi hivyo wanaweza kufanya vizuri Zaidi yao.

“Naamini kwa kutupokea huku na kukubali tupitie vitega uchumi vyenu ili tuone wenzetu mmefanya vitu gani kwani kimapato mpo juu, tunawapongeza sana na tumeona mmestahili kuwa Manispaa na naamini kwa kijifunza huku tunaweza kufanya vizuri zaidi yenu.” Amesema Mbunde.

Aidha kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Michael Waluse, amesema kuwa uamuzi walioufanya wa kujenga kituo cha kisasa cha mabasi Msamvu ni chanzo kikubwa cha mapato kwenye Halmashauri

“Tumeamua kujenga Kituo cha kisasa na ni chanzo kikubwa cha mapato kwenye Halmashauri yetu, hivyo Halmashauri ina mpango wa kufunga mitambo ya kisasa ya kukusanya mapato kwa sababu hili ni eneo ambalo linahitaji ufatiliaji wa karibu sana, ndio maana tutafunga mitambo ya kisasa.” Amesema Waluse.

                        

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.