Header Ads

COSOTA KWA KUSHIRIKIANA NA BODI YA FILAMU TANZANIA YAANZA KUHAKIKI KAZI ZA WASANII KUELEKEA TUZO MPYA ZILIZOANZISHWA NA SERIKALI.

 Afisa COSOTA, Yusuph Chimbongwe,akizungumza juu ya Tuzo za Bodi ya Filamu Tanzania.

TAASISI  ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kwa kushirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania , wameanza zoezi la uhakiki wa kazi za Wasanii kwa ajili ya maandalizi ya Tuzo za Bodi ya Filamu Tanzania ikiwa ni mara ya kwanza Serikali kuanzisha Tuzo hizo.

Uhakiki wa kazi za Wasanii umefanyika leo Septemba 13/2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu.

Akizungumza juu ya maandalizi ya kukusanya kazi za Wasanii, Afisa COSOTA, Yusuph Chimbongwe, amesema lengo la kukusanya kazi za wasanii ni kutaka kujua kama kazi hizo ni za kwao na wameziandaa wenyewe ili kukwepa kutotenda haki wakati wa Tuzo.

"Tupo hapa kwa ajili ya kuona kazi za wasanii, tumewaita ili tukusanye kazi zao , tukiamini kazi tunazo kusanya zimetengenezwa na wasanii husika kwani shindano hili la Tuzo tunataka kutoa washindi ambao wataendana na kazi zao tusipo hakiki tunaweza kukosa usahihi au uhalali wa kazi za msanii tukajikuta yule asiye stahiki akapata tuzo na anayestahiki akakosa" Amesema Chimbongwe.

Chimbongwe, amesema filamu zitakazo pokelewa ni zile ambazo ziliwahi kuwania tuzo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021  lakini zilikosa  tuzo lakini bado zina ubora  basi wao watazichukua na kwenda kuzifanyia kazi.

"Tunajua zipo kazi ambazo tunaweza kutana nazo lakini hazina hati miliki, basi sisi kama COSOTA tutakuwa na utaratibu wetu wa kuhakikisha kazi hizo zinapatiwa hati miliki " Ameongeza Chimbongwe.

Mwisho, amesema baada ya kutoka Mkoa wa Morogoro wanatarajia kufika Mkoa wa Mbeya siku ya Jumatano, na kumalizia Mkoa wa Dodoma Siku ya Ijumaa  huku akisema kuwa shindano la Tuzo hizo za kuwasaka wasanii lenye vipengele mbalimbali linatarajiwa kufanyika Novemba 6/ 2021 katika Jiji la Dar Es Salaam.

Kwa upande wa Msanii wa Filamu Mkoa wa Morogoro, Jayloce Prosper maarufu kama "J"  ameipongeza Serikali pamoja na COSOTA na Bodi ya Filamu kwa kuanzisha Tuzo huku akisema ujio wa tuzo hizo utaleta heshima katika Tasnia ya Sanaa hapa nchini na kufanya Soko la Sanaa kupiga hatua zaidi.




No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.