Header Ads

MANISPAA YA MOROGORO YAANZISHA JUKWAA LA VIJANA.

Afisa Vijana Manispaa ya Morogoro, Jackline Mushi, akizungumza na Vijana waliojitokeza katika mchakato wa uundwaji wa Jukwaa la Vijana Manispaa ya Morogoro.

Afisa Maendeleo kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Rutahiwa John, (kulia) akizungumza wakati wakutoa semina kwa Vijana.

Mkurugenzi wa M2 Smart CO.LTD  Kikundi cha uzoaji taka, Ismail Hamad (kulia) akifuatilia kwa umakini Kikao cha uundwaji wa Jukwaa la Vijana Manispaa ya Morogoro.

Afisa Vijana Manispaa ya Morogoro, Jackline Mushi, (watatu kutoka kushoto) akiwa pamoja na Viongozi wa mpito waliochaguliwa kwa ajili ya mchakato wa uundwaji wa Jukwaa la Vijana Manispaa ya Morogoro.

Kwa muda mrefu kumekuwepo na pengo la taarifa kuhusiana upatikanaji na utolewaji wa fedha za Mifuko wa Vijana ni moja ya changamoto inayo warudisha nyuma Vijana wengi wenye ndoto na malengo ya kuikomboa jamii inayo wazunguka.

Manispaa ya Morogoro  wameanza mchakato wa kuunda Jukwaa la Vijana ikiwa na lengo la kumkomboa Kijana kifikra na kujitambua .

Kikao hicho kilichojumuisha Vijana kutoka katika kanda mbalimbali zilizopangwa kutoka katika vikundi vyao vilivyopatiwa Mkopo na Manispaa  , kimefanyika leo Septemba 08/2021  katika  Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingalu, 

Akizungumza na Vijana hao,  Afisa Vijana Manispaa ya Morogoro, Jacklin Mushi, amesema lengo la Jukwa hilo la Vijana linalenga kupashana habari lakini pia kupeana Maarifa ya namna gani vijana wanavyoweza kutumia rasilimali zilizopo kujikwamua na hali ya maisha. 

Mushi, amesema kumekuwa na tabia ya vijana wengi kupenda kujiachia na kutokutafiti kuhusu masuala yanayowahusu huku akisisitiza na kusema ni muhimu sasa Vijana waamke na kujikwamua wenyewe maana hakuna mtu hatakaye wapigania kama wao wamelala.

 “kuanzishwa kwa jukwaa hili kwenye Halmashauri yetu ya Manispaa ya Morogoro , itachangia kujitambua kwa Vijana na kujiajiri kwenye shughuli mbalimbali" Amesema Mushi. 

Katika hatua nyengine, Mushi,amesema kuwa  Manispaa ya Morogoro ,imetenga mikopo isiokuwa na riba kwa lengo la kuwainua Vijana kiuchumi, na amesisitiza Vijana kuchangamkia Fursa hiyo.

Kuhusu suala la mkopo kwa Vijana , Mushi ,amesema kuwa  vigezo vya kupata mikopo sio rahisi ila inahitaji mtu kwanza aelewe fika nini anataka kufanya kabla ya kuomba fedha za Mfuko wa Vijana. 

"Upatikanaji wa fedha hizi za mkopo  kinadharia ni mwepesi kweli kwa kuwa pesa mnayo kwenda kuomba inatokana na sisi wenyewe walipa kodi ila ni lazima upitie njia ndefu kidogo na uaminike jambo ambalo sasa linakuwa gumu kwa vijana wengi" Ameongeza Mushi.

Mwisho, Mushi, amesema  kuwa  dira ya Manispaa  ya Morogoro kwa sasa ni kuwawezesha Vijana kiuchumi, Kutoa elimu juu ya madhara yanayotokana na madawa ya kulevya na kuwapa mikopo isioyokuwa na riba kwa lengo la kuwawezesha Vijana kiuchumi.

Naye Afisa Maendeleo kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro , Rutahiwa John, amewasihi vijana kufikiri Zaidi baada ya kuishia kwenye mawazo na kushindwa kutekeleza malengo yao au wengine kuishia katika kulalamika na kuwalaumu viongozi.

Rutahiwa, amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, inaendelea  na Jitihada mbalimbali za kuwezesha Vijana kiuchumi na kuwapatia mikopo kwa lengo la kuwawezesha vijana waweze kujiajiri na sio kutegemea ajira.

Kwa upande wa mmoja wa Vijana waliohudhuria katika Kikao hicho, ambaye pia ni Mkurugenzi wa M2 Smart CO.LTD  Kikundi cha uzoaji taka, Ismail Hamad, ameushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuanzisha Jukwaa la Vijana.

Ismail , amesema kuwa wao kama Vijana watahakikisha mpango huo unafanikiwa na watakuwa mstari wa mbele kuona Jukwaa hilo linafikia malengo yake na vijana kuweza kunufaika.

No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.