MKUU WA WILAYA MOROGORO AFANYA ZOEZI LA UGAWAJI WA VIBANDA VYA BIASHARA KWA MACHINGA.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, akizungumza na Machinga Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga (kulia), Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Ally Hamu Machela (wapili kutoka kulia), Diwani wa Kata ya Mafiga, Mhe. Thomas Butabile (kushoto), Diwani Viti Maalum, Mhe. Salma Mbando (wapili kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja Mkutano wa Mkuu wa Wilaya wa kugawa Vibanda kwa Machinga Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
MKUU wa Wilaya ya Morogoro Mh. Arbert Msando amefanya zoezi la ugawaji wa vibanda vya kufanyia biashara kwa Machinga Manispaa ya Morogoro.
Zoezi hilo limefanyika septemba 14, 2021 soko
kuu la Chifu Kingalu mkoa wa Morogoro.
Katika zoezi
hilo Mh. Msando amesema kuwa kufanyika kwa zoezi hilo ni katika kutekeleza
agizo la serikali kuwatengea maeneo ya biashara wamachinga ili waweze kufanya
biashara zao maeneo rafiki.
“Katika
kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan, wilaya yangu tutawagawia maeneo ambayo tumeyatenga rasmi kwa ajili ya
wamachinga kwa kufuata utaratibu mzuri ambao hautomuathiri yeyote, lengo ni
kutatua kero ya mda mrefu ya machinga katika Wilaya ya Morogoro kwa kuhakikisha
machinga wote wanapata heshima na kuthaminiwa kama watu wengine na sio watu wa
ziada kama ilivyozoeleka.” Amesema DC Msando.
Ameongeza kuwa
masuala yaliyowatatiza wamachinga kwa mda mrefu kwa kutokua na eneo la kudumu
la kufanyia biashara sasa limekwisha na
kuwa watamiliki maeneo hayo kwa halali, na kwa uwazi kabisa na kwa kujua katika
kufanya biashara kwenye maeneo hayo kipi hawapaswi kulipa na kipi wanapaswa
kulipa na kwa kiasi gani.
Pia katika utekelezaji
wa zoezi hilo DC Msando amesema kuwa
aliyekuwa na Cheo chochote au Mtendaji yeyote anatakiwa ajue Mmachinga sio mtu
wa ziada bali ni Mwanachi wa kawaida kama wengine.
“Viongozi wote
na Watendaji wote wajibu wenu ni kuwasaidia na kushirikiana nao hao Machinga,
kwani wewe ni mtumishi na mhudumu wa wananchi hivyo yote mnayoyapanga yaoneshe
kwamba ninyi mnawatumikia wananchi hawa, mnawatetea wananchi hawa, mnasimama na
wananchi hawa, muwasaidie na mtambue ya kuwa hao sio watu wa ziada katika
wilaya hii bali ni wanachi wa kawaida kama wengine hivyo tushirikiane nao na
wapeni tozo ambayo inalipika kwenye maeneo haya.”Ameongeza DC Msando.
Kwa upande wake
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mh. Kalist Lazaro, ambae amehudhuria utekelezaji wa
zoezi hilo alipopata fursa ya kuja kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa
Kassim, amesema kuwa amekuja kujifunza nae ataiga kufanya hivyo kwenye wilaya
yake.
“Nilipopata
fursa ya kuja Morogoro kwenye ziara ya Waziri nikaona niitumie nafasi hii kuja
kujifunza, na mimi nitaiga ili tumsaidie Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, tumeteuliwa ili tutatue kero za wananchi.”Amesema DC Lazaro.
DC Lazaro, amewaomba
viongozi wa machinga kuacha kutumika kisiasa katika utekelezaji wa haki za
machinga, bali washirikiane nao na kuwasaidia wamachinga.
“Niwaombe
viongozi wa Machinga kuacha kutumika kisiasa, mshirikiane na muwasaidie wamachinga,
Pia ninyi viongozi na wamachinga wote ondoeni uadui na Halmashauri kwa
kushirikiana nao na nyinyi machinga msiuze hivi vibanda kwani ndo hazina yenu
kwa siku zijazo.” Ameongeza DC Lazaro.
Katika zoezi
hilo Mh. Msando amesema kuwa lazima wamachinga wahakikishiwe kwa maandishi ya
kisheria kwamba maeneo hayo ni maeneo yao ya kudumu, pia wamachinga wawe na
vikundi vyao ambao vitasajiliwa kama vikundi rasmi na manispaa ambavyo vitawasaidia
wao kulinda na kutetea haki zao wenyewe ili kuepuka usumbufu wa aina yeyote na
kama kuna changamoto tunakutana nazo inatakiwa kutatuliwa kwa kufuata taratibu.
Post a Comment