Header Ads

MBUNGE ABOOD AKABIDHI MADAWATI 1000 YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 52 KWA SHULE ZA MSINGI MANISPAA YA MOROGORO.

 

Mhe. Abood (kulia) akimkabidhi Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Nanenane Kata ya Tungi, Hundi yenye thamani ya shilingi Laki 4 na 90 elfu kwa ajili ya kulipia bili ya maji .


MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood, amekabidhi  madawati 1000 yenye thamani ya Shilingi Milioni 52 kwa shule za Msingi Manispaa ya Morogoro ili kukabiliana na upungufu wa madawati uliosababishwa na ongezeko kubwa la usajili wa wanafunzi.

Madawati hayo yaliyotengenezwa kupitia mfuko wa Jimbo yamekabidhiwa kwa Kaimu  Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro , Mayasa Mwinyi , kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro.

 “Hii ni hatua ya awali ya kuchangia madawati haya kupitia mfuko wa Jimbo,lakini tayari tumeanza kuwatafuta wadau mbalimbali watuunge mkono kutatua changamoto hii ya upungufu wa madawati Jimbo la Morogoro Mjini, nami  kwa upande wangu nitahakikisha nashirikiana na viongozi wenzangu na wadau mbalimbali wa Maendeleo ili mwanafunzi wa Jimbo la Morogoro Mjini asome katika mazingira ambayo ni rafiki”Amesema Abood.

Nitoe rai kwa mashirika,Taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo kutuunga mkono kwenye jambo hilo jema na kutekeleza maelekezo ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanafunzi hawakai chini.

Kwa upande wa Kaimu  Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro , Mayasa Mwinyi , ametumia  fursa hiyo kumshukuru Mbunge  Abood na kamati ya Mfuko wa Jimbo kwa kuunga mkono jitihada za Manispaa ya Morogoro za utengenezaji madawati 1000  ili kupunguza na kuondokana  na changamoto hiyo ya upungufu wa Madawati katika shule za msingi.

Akitoa shukrani, Diwani wa Kata ya Mkundi, Mhe. Seif Chomoka,  amemshukuru Mbunge Abood  kwa kuwa mstari wa mbele kwenye kutatua changamoto za sekta ya Elimu na kuahidi kushirikiana nae kwenye kuhakikisha wanafunzi wa Kata ya Mkundi na Manispaa kwa ujumla  wanasoma katika mazingira rafiki ili kuchochea ufaulu wa wanafunzi katika Jimbo la Morogoro Mjini.

Katika hatua nyingine , wananchi pamoja na Wazazi wa wanafunzi Manispaa ya Morogoro wamemshukuru  Mbunge Abood  na Uongozi wa Manispaa ya Morogoro ikiwemo Madiwani wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Hamu Machela  kwa jinsi wanavyopambana na changamoto za elimu ikiwamo changamoto za Madawati.

Miongoni mwa shule zilizopokea Madawati katika awamu hii ya kwanza ambapo kila shule imepokea madawati 50 ni pamoja na Shule za Msingi Chamwino A na B na Kambarage Kata ya Chamwino , Shule ya Msingi Juhudi Kata ya Lukobe, Shule ya Msingi Kiegea Kata ya Kihonda, Shule ya Msingi Nanenane Kata ya Tungi, Shule ya Msingi Kikundi Kata ya Sultan Area, pamoja na Shule ya Msingi Kilongo Kata ya Mkundi.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.