MWALIMU NYERERE AENZIWE KWA VITENDO-DC MSULWA.
MKUU wa Wilaya ya
Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amewataka Wananchi pamoja na Viongozi mbalimbali
kumuenzi Hayati Baba wa Taiafa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.
Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 14, 2020 , wakati wa Tamasha la
kumuenzi Mwalimu Nyerere lililofanyika kwenye Viwanja vya Mnada wa Nyama Choma
Nanenane Kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari,amesema
kuwa kumbukumbu za Baba wa Taifa zina mambo mengi ya kujifunza ambayo wananchi,
viongozi pamoja na wanasiasa wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo hasa kuwa
wazalendo kwa nchi, uvumilivu, kudumisha upendo na moyo wa kujitoa kwa dhati
kuwatumikia wananchi.
“Kupitia kumbukumbu hizi sisi watumishi wa Umma, Wananchi , Viongozi
mbalimbali pamoja na Wanasiasa , tunatakiwa kujifunza ukomavu wa demokrasia
aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la Afrika, wengi
wanadhani Demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe demokrasia ni pamoja na
kuheshimu watu wengine, leo ni miaka 21 tangia atutoke Kipenzi chetu lazima
tujitafakari dhdi ya kauli zake alizotuachia Baba wa Taifa, ” Amesema DC Msulwa
.
DC Msulwa, ameeleza kuwa maisha
aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na watanzania wote hasa
pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la Afrika alipoepuka tamaa ya
madaraka na mali kwa manufaa ya taifa.
“Sote ni mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa
anaishi mwalimu kabla hajajengewa nyumba na Jeshi kama Rais mstaafu wengi
walitegemea asingeishi katika eneo lile, kumbukumbu hii nzuri aliyoiacha
inatufundisha watanzania kuwa mwalimu aliitanguliza Tanzania mbele kuliko
maslahi yake binafsi, sasa haya ambayo tumeyaona yanatufundisha nini tukifanye
kwa Taiafa letu ili liweze kupiga hatua mbele
” Amesisitiza DC Msulwa.
Aidha, DC Msulwa, amebainisha
kuwa Wilaya yake kwa kushirikiana na Viongozi wa Halmashauri wataendelea kumuenzi Baba wa Taifa kwa yale aliyoyafanya
na kuyasimamia kwa manufaa ya taifa huku akitoa wito kwa viongozi mbalimbali wawe na kiasi na waridhike na vile
walivyonavyo.
“Suala la kuridhika na kuwa na kiasi linapaswa kuzingatiwa, Viongozi wanapaswa kuwaheshimu wananchi na kipindi hiki
tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 28,2020 , niwaase Wanasiasa wafanye
Kampeni za kistaarabu na kuwaheshimu wale ambao wanawachagua kupitia chaguzi mbalimbali, matokeo yanapotoka
kama ni sahihi basi wanasiasa wakubaliane na maamuzi yao na sio kleta fujo
ambazo zitakuwa na matokeo mabaya kwa Jamii na kutia doa Taiafa letu
linaloongoza kwa amani Duniani kote ” Ameainisha DC Msulwa.
Kwa upande wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mstaafu, Mhe. Steven
Mshishanga, amesema kuwa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere alikuwa ni mtu wa kipekee kwa viwango vya Afrika na dunia kutokana na
kumbukumbu ya uadilifu aliyoiacha ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mashishanga, amesema kuwa
Mwalimu Nyerere alipigania uhuru wa nchi za Afrika na haki ya kijamii ambapo
alikuwa kielelezo cha uongozi kwa nchi zote za Afrika katika mapambano yao ya
uhuru na hamu ya amani, uhuru na maendeleo ya kiuchumi.
“Kama kiongozi mwenye busara, Mwalimu alichangia sana katika mjadala kuhusu pengo la maendeleo ya kiuchumi baina ya mataifa ya Kaskazini na yale ya Kusini mwa dunia, kwa hiyo niwapongeze sana Uongozi wa Wilaya na Manispaa kwa kunialika hapa na kufanya tukio kubwa kama hili, Hafla ya leo ni muhimu, kwani Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye uadilifu, ujasiri na shujaa wa uhuru wa Afrika” Amesema Mashishanga.
Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kuwa watanzania wanayo mengi ya kujifunza kupitia vitu alivyoviacha Baba wa Taifa ambavyo vimehifadhiwa katika Makumbusho hivyo wana kila sababu yakujifunza zaidi.
Lukuba ,amesema kuwa maisha ya uadilifu aliyoishi enzi za uhai wake na mchango wake katika kuiletea maendeleo Tanzania na Bara la Afrika vinapaswa kuenziwa kwa nguvu zote na viongozi wa Tanzania.
Sherehe hizo za kumbukizi za Mwalimu Nyerere, zilihududhuriwa na Viongozi mbalimbali ikiwemo Viongozi wa vyama vya Siasa ambapo katika Tamasha hilo liliambatana na Uzinduzi wa Mnada wa Nyama choma Nanenane Kata ya Tungi ambapo wasanii mbali mbali walitoa burudani ikiwamo Msanii wa Singeli Msaga Sumu pamoja na Wasanii wa ndani wa Manispaa ya Morogoro wakiongozwa na MC Hamza.
Mnada wa Nyama Choma utakuwa ni endelevu ambapo utakuwa unafunguliwa kila Jumapili kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi 112:30 jioni.
Post a Comment