Header Ads

Abood awaahidi makubwa Wananchi wa Jimbo la Morogoro Mjini.

        

Mgombea Ubunge, Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood (kushoto), akimnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Kilakala, Ndug. Marco Kanga (kulia)  kwenye Uwanja wa Ikweta Kata ya Kilakala.

    




MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kuptia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Abdulaziz Abood, amewahakikishia wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwa ,serikali ya awamu ya tano imejipanga kumaliza changamoto zote zinazowakabili ikiwemo ya upatikanaji wa huduma bora  ya maji safi na salama endapo watawapatia ridhaa tena ya kuongoza katika kipindi cha miaka 5 ijayo.

Ameyasema hayo Oktoba 04,2020, wakati wa muendelezo wa  Kampeni yake kwenye Viwanja vya Ikweta Kata ya Kilakala. akimnadi  wa udiwani wa Kata ya Kilakala, Ndug Marco Kanga,  ambapo amewataka wananchi wa kata hiyo kumchagua diwani huyo ili aweze kuwaletea maendeleo.

Abood, amesema kuwa  siku zote kitu ambacho alikuwa akikipigania kwa nguvu zote alipokuwa  Bungeni ni kuhusu tatizo la maji katika Manispaa ya Morogoro ambapo sasa Serikali imetambua jambo hilo na kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji.

Amesema kuwa amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kutoa msaada wa fedha hizo baada ya kuona juhudi kubwa alizozifanya kwa kushirikiana na  Uongozi mzima, Chama Cha Mapinduzi,  Wilaya na   mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro katika  kuleta maendeleo.

“ Binafsi nikiwa bungeni nimebatizwa jina la bwana maji, maana kila nikisimama nazungumzia maji, kwakuwa ninajua tatizo kubwa kwa wananchi wangu ndio hilo, naombeni mtupe ridhaa tena katika miaka 5 ijayo ili tuendelee kuwatumikia ” Amesema Mhe. Abood.

“ Nashukuru sasa tayari serikali imeshanielewa , na tumepata mradi mkubwa wa maji na tayari mkandarasi alishasaini  kuanza kazi mara moja na muda si mrefu tutaondokana na tatizo hili” Ameongeza Mhe. Abood.

Kuhusu hospitali ya wilaya alisema, amewasiliana na Waziri wa TAMISEMI  na amehamikishia kuwa zitatolewa fedha kwa ajili ujenzi wa wodi ya kisasa, chumba cha upasuaji na nyumba ya mganga ili iweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa kata zilizopo pembezoni mwa Manispaa .

Mbunge huyo alisema , licha ya kuchangia ujenzi wa zahanati kila kata ,amewalipia bima ya afya (CHF iliyoboreshwa ) wazee wote kila kata ili kupata huduma za matibabu katika zahanati na vituo vya afya.

Kuhusu sekta ya elimu alisema , ametoa mifuko 100 ya saruji na nondo kwa kila darasa linalojengwa kila kata ili kumaliza changamoto ya upungufu wa madarasa.

Kwa upande wa Mgombea Udiwani wa Kata ya Kilakala , Marco Kanga, amempongeza sana Mhe. Abood katika kipindi chake cha miaka 5, shughuli za kimaendeleo zimefanyika na kukamilishwa ikiwemo kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa , kujengwa barabara za kiwango cha lami na kuiwezesha Manispaa kuwa na sifa ya kuelekea kuwa Jiji.

Hivyo amesema  katika kuboresha huduma za usafiri ,atakapopata ridhaa atahakikisha barabara zote za mitaani zinakuwa bora kwa ajili ya kutoa huduma bora za usafiri.

Kanga, amesema akichaguliwa, atahakikisha anawaunganisha Vijana, Wakina Mama na watu wenye ulemavu wajiunge vikundi ili waweze kupata mikopo ya Ujasiriamali inayotolewa na Manispaa.

Kuhusu Sekta ya Afya, atahakikisha kwamba anasimamia Wazee kuwe  kupatiwa vitambulisho kwa ajili ya kupatiwa huduma za afya bure.

Pia, atahakikisha kila mambo yanayohusu maisha ya wana Kilakala, watashirikiana kikamilifu na kupokea maoni ya Wananchi ili kuijenga Kilakala kwa pamoja.


No comments

Theme images by A330Pilot. Powered by Blogger.